Bariadi,
Makatibu Tawala wasaidizi,wakuu wa vitengo pamoja na Maafisa katika Ofisi ya katibu Tawala Mkoa wa Simiyu wameanza kupatiwa mafunzo ya Mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma kielektroniki NeST ili waweze kufanya manunuzi kupitia mfumo huo mpya ulioboreshwa zaidi.
Kaimu katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Bw.Majuto Njanga ameyafungua mafunzo hayo ya siku 4, yaliyoanza kutolewa katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Simiyu ambapo amewataka washiriki kufuatilia kwa makini mafunzo hayo ili Mkoa uweze kutumia mfumo wa NeST kwa wakati kulingana na maelekezo yaliyotolewa na Serikali.
Bw.Njanga amewaambia washiriki wa mafunzo hayo kuwa mfumo wa Nest utakapoanza kutumika utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya rushwa pamoja na kuongeza uwajibikaji baina ya watumishi wa Umma katika Taasisi za Serikali.
Amewataka Makatibu Tawala wasaidizi pamoja na wakuu wa vitengo ofisini hapo kuteua watumishi sahihi kutoka kwenye Idara zote kama miongozo inavyoelekeza katika matumizi sahihi ya Mfumo mpya wa NeST.
Agosti 1 Hadi 5 ,2023 Wataalamu 6 kutoka Ofisi ya katibu Tawala Mkoa wa Simiyu walishiriki mafunzo mjini Dodoma ya kuwajengea uwezo kuwa wawezeshaji wa Mfumo mpya wa NeST yalitolewa na PPRA
Mafunzo ya Mfumo wa NeST yatatolewa pia kwa watumishi wa ngazi ya Halmashauri Mkoani Simiyu ili waweze kuanza mara moja kutumia Mfumo huo mpya wa ununuzi wa Umma.
Awali Serikali ilikuwa ikitumia mfumo wa TANEPS katika ununuzi wa Umma ambao ulibainika kuwa na changamoto mbalimbali hatua iliyopelekea Serikali kuachana na mfumo wa zamani na kuja na Mfumo mpya wa NeST ili kurekebisha changamoto zilizojitokeza na kuboresha Mfumo mzima wa ununuzi wa Umma Nchini.
GCO,
Simiyu -RS
17 Agosti 2023.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa