KWA NINI UWEKEZE MKOANI SIMIYU
Utangulizi.
Simiyu ni miongoni mwa mikoa mipya hapa nchini. Mkoa wa Simiyu una eneo la kilomita za mraba 23,807.7 ambazo ni sawa na hekta23,807,700. Mkoa huu unatimiza miaka 13 mwaka huu wa 2025 tangu ulipoanzishwa mwaka 2012. Hivyo Simiyu ni miongoni mwa mikoa michanga Nchini, kwa hiyo unapaswa kutazamwa kwa namna ya kipekee kibiashara na kiuwekezaji.
Mkoa wa Simiyu unaunganishwa kwa urahisi na nchi za Kenya, Uganda, Burundi,Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Zifuatazo ni miongoni mwa sababu za kuwekeza Mkoa wa Simiyu;
Hali nzuri ya Hewa.
Mkoa huu unafaa kwa uwekezaji kwa sababu ya hali nzuri ya hewa, ambayo ni nzuri kwa shughuli za utalii, kilimo na ufugaji. Hali ya mvua kwa mwaka ni wastani wa kati ya 600mm hadi 900mm. Katika baadhi ya maeneo (Meatu) kiasi cha mvua ni 400mm. Hali ya joto ni kati ya 18°C hadi 31°C. Kwa ujumla, kuna misimu miwili ya mvua; msimu wa mvua za vuli kati ya mwezi Oktoba hadi Desemba na ule wa masika kati ya miezi ya Februari na Mei kila mwaka.
Amani na utulivu.
Serikali Mkoani Simiyu imeimarisha hali ya Ulinzi Pamoja na usalama wa raia na Mali zao. Amani na utulivu wa kisiasa ambavyo hujenga mazingira ya usalama pamoja na kiwango cha chini cha uhalifu ni vivutio vingine vya kumfanya mtu awekeze katika mkoa huu.Wawekezaji hawana haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa mali zao watakazowekeza katika mkoa huu.
Ardhi yenye rutuba.
Mkoa wa Simiyu umebarikiwa kuwa na Ardhi yenye rutuba kwa ajili ya shughuli za Kilimo ikiwemo uzalishaji wa mazao mbalimbali ya biashara na chakula.Ardhi ya Mkoa wa Simiyu ni rafiki kwa kilimo cha mazao ya Biashara kama vile Pamba,Karanga,Alizeti na Mkonge ambapo mazao ya chakula ni Pamoja na Mahindi,Mpunga,Mtama,Muhogo,ulezi na Viazi vitamu.
Idadi ya watu.
Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Simiyu ulikuwa na jumla ya watu 2,140,497; Wanaume wakiwa 1,034,681 na Wanawake 1,105,816. Shughuli kuu ya kiuchumi Mkoa wa Simiyu ni Kilimo na ufugaji, zao la pamba inachangia zaidi ya asilimia 60% ya pamba yote inayopatikana Tanzania.Idadi ya watu Mkoani Simiyu inatoa fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza Mkoani Simiyu katika Sekta mbalimbali kutokana na uwepo wa fursa ya Soko la Uhakika la bidhaa mbalimbali.
Miundombinu Rafiki ya uchukuzi.
Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ya Uchukuzi kwa lengo la kuimarisha huduma kwa Wananchi pamoja na kujenga mazingira wezeshi kwa usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali ili kukuza uchumi katika Mkoa wa Simiyu na kuchochea mazingira bora kwa wawekezaji.
Kupitia Wakala ya Barabara TANROADS katika Mkoa wa Simiyu Serikali inaendelea na ukarabati na kufanyia matengenezo mtandao wa Barabara wenye urefu wa jumla ya Kilomita 925.54 na jumla ya madaraja 366.
Barabara hizi ni za aina kuu mbili, barabara kuu na barabara za mkoa na pia ipo barabara moja ya Wilaya ambayo TANROADS imekasimiwa. Barabara kuu zina jumla ya kilometa 333.04, kati ya hizo kilometa 213.51 ni lami na kilometa 119.53 ni za changarawe. Barabara za lami ni asilimia 25.2 ya barabara zote na zilizobaki asilimia 74.8 ni za changarawe.
Barabara za mkoa zina jumla ya kilometa 525.51, kati ya hizo barabara za changarawe ni kilometa 506.19.
Barabara ya Wilaya iliyokasimiwa TANROADS ina urefu wa kilometa 66.99 yaNkoma – Makao hadi Ndutu inayounganisha mkoa wa Arusha kupitia Karatu. Barabara hii ya kiwango cha changarawe ni nzuri inapitika kwa majira yote ya mwaka. Barabara hii ni muhimu sana kwa mkoa wa Simiyu kwani ni lango kuu la kuingia mbuga tengevu ya Maswa (Maswa Game Reserves) ambayo inaunganisha mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro.
Mtandao wa Barabara mkoa wa Simiyu unaunganaisha mikoa mitano (5) majirani ya Singida, Shinyanga, Mwanza, Mara na Arusha lakini pia tunapakana na ziwa viktoria kwa upande wa Wilaya ya Busega. Aidha barabara hizi zinaunganisha Wilaya tano (5) za kiutawala zilizopo ndani ya mkoa wa Simiyu.
Maboresho haya ni kichocheo kikubwa kwa wawekezaji kuja kuwekeza ndani ya Mkoa wa Simiyu kutokana na miundombinu ya uhakika ya uchukuzi.
Ujenzi wa kituo cha Abiria cha Reli ya Kisasa unaondelea katika eneo la Malampaka utatoa fursa kwa wawekezaji kurahisisha shughuli za uchukuzi wa abiria na bidhaa kutoka Mji wa Kibiashara Dar es salaam,pamojana makao makuu ya Nchi Dodoma
Kuimarika kwa Sekta ya Maji Mkoani Simiyu.
Serikali Mkoani Simiyu imeendelea kuimarisha na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji, kutoka asilimia 60.85 Novemba 2020 hadi asilimia 71 Aprili 2025. Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini-RUWASA imeendelea kutekeleza Miradi 26 ambayo utekelezaji wa miradi hiyo iko kati ya asilimia 20 hadi 95.
Nishati ya uhakika;
Wilaya zote tano za Mkoa wa Simiyu zimeunganishwa kwenye gridi ya Taifa. Wilaya hizo zinapata umeme wake kutoka Gridi ya Taifa kupitia kituo cha kupoza umeme cha Nyakato na Mabuki Mkoa wa Mwanza, kituo cha Bunda Mkoa wa Mara na Ibadakuli Mkoa wa Shinyanga. Matumizi ya juu ya Mkoa wa Simiyu ni Megawati 13.7. Sekta ya umeme imetekeleza jumla ya miradi ipatayo 12. Kwa uchache miradi mikubwa iliyotekelezwa ni: Mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili kupeleka umeme kwenye vijiji 201, Mradi wa umeme migodini kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu, Mradi wa UVIKO kupeleka umeme kwenye visima vya maji 10 na Mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Mkoa wa Simiyu kwa gharama ya shilingi bilioni 97. Wakandarasi wapo wanaendelea na utekelezaji wa miradi ya umeme katika ngazi ya Vitongoji, Aidha vitongoji vilivyokuwa na umeme ni 269 kuanzia Novemba, 2020 na vimeongezeka hadi kufikia Vitongoji 971 Aprili, 2025.
Mafanikio haya katika Sekta ya Nishati yanaufanya Mkoa kuwa sehemu rafiki kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika Sekta ya Viwanda pamoja na huduma mbalimbali za Kijamii.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa