Mkoa wa Simiyu ulianzishwa kwa Tangazo la Serikali (GN) Na. 72 la tarehe 02 Machi, 2012. Mkoa huu unapatikana Kaskazini mwa Tanzania, Kusini Mashariki mwa Ziwa Victoria. Mkoa huu upo kati ya longitudo 33°03” na 34°01” Mashariki ya mstari wa Griniwichi na latitudo 02°01” hadi 04°00” Kusini mwa Ikweta. Kwa upande wa Kaskazini, Mkoa wa Simiyu unapakana na Mkoa wa Mara; upande wa Mashariki Mikoa ya Arusha Singida na Manyara; Kusini Mkoa wa Shinyanga na Tabora na upande wa Magharibi Mkoa wa Mwanza.
Mkoa wa Simiyu una eneo la kilomita za mraba 23,807.70. Eneo linalofaa kwa shughuli za kilimo na ufugaji ni kilomita za mraba 11,479.10 kilomita za mraba 11,723.60 ni eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mbuga ya Serengeti, Mapori ya Akiba ya Maswa, Kijereshi na Mwiba; na Hifadhi za Jumuiya za Wanyama Pori ya Makao (WMAs) iliyoko katika Wilaya ya Meatu na kilometa za mraba 605 ni eneo la maji ya Ziwa Victoria.
Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002, Mkoa wa Simiyu ulikuwa na jumla ya watu 1,584,157; Wanaume wakiwa 759,891 na Wanawake 824,266. Mkoa una ongezeko la watu wa wastani wa asilimia 1.8 kwa mwaka.
Hali ya mvua kwa mwaka ni wastani wa kati ya 600mm hadi 900mm. Katika baadhi ya maeneo (Meatu) kiasi cha mvua ni 400mm. Hali ya joto ni kati ya 18°C hadi 31°C. Kwa ujumla, kuna misimu miwili ya mvua; msimu wa mvua za vuli kati ya mwezi Oktoba hadi Desemba na ule wa masika kati ya miezi ya Februari na Mei kila mwaka.
Mkoa wa Simiyu unaundwa na Wilaya tano (5) zenye majimbo saba (7) ya Uchaguzi wa Ubunge (Itilima, Bariadi, Maswa Mashariki, Maswa Magharibi, Busega, Kisesa na Meatu); na Halmashauri sita (6). Aidha, kuna Tarafa 16, Kata 130, Vijiji 471 na Mitaa 92
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa