Pichani:Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Awesu pamoja na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wakishuhudia utiaji saini mkataba wa utekelezaji Ujenzi wa Miundombinu ya Maji,Mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi Mkoani Simiyu 27 Mei 2023 katika eneo la Stendi ya Zamani ya Mji wa Bariadi.
Na IO.Simiyu
Wakazi wapatao 494,000 wa Mkoa wa Simiyu watanufaika kupitia Mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi unaohusisha Ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa Maji Ziwa Viktoria na kuyapeleka katika Wilaya za Busega, Bariadi, Lagangabilili, Maswa na Meatu na vijiji vilivyoko pembezoni mwa bomba kuu utakapopita mradi huo.
Tarehe 27 Mei 2023 Wizara ya Maji ilisaini mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya maji, mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi mkoani Simiyu ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandishi Nadhifa Kemikimba na Kampuni ya M/S China Civil Engineering Construction Cooperation CCECC LTD kutoka China ambayo imewakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa kampuni hiyo Bw. Wu Zegang walisaini Mkataba huo huku Waziri wa Maji Nchini Mhe.Jumaa aweso akishuhudia utiaji Saini wa Mkataba huo.
Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb) katika hotuba yake aliwahakikishia Wananchi wa mkoa wa Simiyu kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati ili kutimiza adhma ya Serikali kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora ya maji safi na salama.
Alisema mkataba unamtaka mkandarasi atekeleze mradi huo kwa miaka minne hadi Agosti 2025, hivyo Wizara itahakikisha inamsimamia kwa ukaribu ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Dkt.Nawanda alipowahutubia Wananchi wa Mkoa wa Simiyu alimshukuru Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali Wananchi wa Mkoa wa Simiyu ambapo ameeleza kuwa hatua ya Serikali kutia saini mkataba wa Bilioni 440 wa Ujenzi wa Mradi huo utaondoa kabisa changamoto ya uhaba wa Maji Mkoani Simiyu.
Aidha RC Dkt.Nawanda amemhakikishia Waziri wa Maji Mhe.Juma Aweso na Wananchi kwa ujumla kuwa Serikali Mkoani Simiyu itashirikiana bega kwa bega na Wananchi katika kuhakikisha kuwa miundombinu ya mradi huo inalindwa kwa nguvu zote.
Katika hatua nyingine Mhe.Dkt Nawanda emetoa rai kwa Kampuni itakayotekeleza Ujenzi wa Mradi huo kutoa kipaumbele kwa Watanzania hususani Wazawa ili kusudi mradi huo uwe chachu ya Wananchi kujipatia kipato na ajira wakati wa utekelezaji wake.
Fedha za Mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Mkoani Simiyu zimechangiwa na wadau mbalimbali ambapo serikali ya Tanzania inatoa Euro milioni 40.7, sawa na shilingi za Tanzania Bilioni 105.8. Serikali ya Ujerumani Euro milioni 26.1 sawa na shilingi za kitanzania Bilioni 67.9, Shirikika la kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (GCF) Euro milioni 102.7 sawa na shilingi za Tanzania Bilioni 267. Mchango wa wananchi kupitia nguvu zao unatarajiwa kugharimu Euro milioni 1.5 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 3.9
MATUKIO MBALMBALI KATIKA PICHA WAKATI WA HAFLA YA UTIAJI SAINI MIKATABA YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MAJI,MRADI WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI
Picha 1.Waziri wa Mji Mhe.Juma Aweso akivalishwa Skafu na Skauti mara baada ya kuwasili katika eneo la Stendi ya Zamani kushuhudia tukio la utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa miundombinu ya Mji,Mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi 27 Mei 2023.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa