Bariadi,
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Bi.Prisca Kayombo amewataka Viongozi wa Dini Mkoani humo kushirikiana na wataalamu wa Afya katika utoaji Elimu juu ya namna ya kudhibiti Ugonjwa wa Malaria.
Bi.Kayombo ametoa rai hiyo katika mkutano wa uraghibishaji ngazi ya Mkoa uliokutanisha Viongozi mbalimbali wa Mkoa, Viongozi wa Dini, wawakilishi wa Waganga wa Tiba Asili pamoja na wadau mbalimbali wa Afya ngazi ya Mkoa na Wizara uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bariadi Conference Wilayani Bariadi,lengo likiwa ni kujadili namna Bora ya utekelezaji wa afua mbalimbali za kukabiliana na Ugonjwa wa Malaria ,ambapo katika mkutano huo kampeni ya ugawaji wa Vyandarua Mkoani humo imezinduliwa rasmi.
Amesema Viongozi wa Dini Mkoani humo wana mchango mkubwa katika kufikisha Elimu ya kukabiliana na Malaria kwa Waumini wao ambapo kufanya hivyo kutasaidia kwa sehemu kubwa Jamii kubadili mitizamo mibaya juu ya baadhi ya Afua za kukabiliana na Malaria ikiwemo matumizi ya Vyandarua.
"Viongozi wa Dini wanayo nafasi kubwa katika kuwaelimisha Wananchi kuachana na Imani potofu ikiwemo dhana iliyojengeka kuwa Vyandarua vyenye dawa vinapunguza Nguvu za kiume"Alisema Katibu Tawala Kayombo.
Aidha amewataka Viongozi hao wa Dini kuhamasisha Wananchi kufanya Usafi wa Mazingira mara kwa mara hatua itakayosaidia kuondoa mazalia ya mbu.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Viashiria vya Malaria Nchini Maambukizi ya Malaria Mkoani Simiyu yameongezeka kutoka asilimia 6 mwaka 2017, hadi kufikia asilimia 11.2 mwaka 2022.
GCO,
Simiyu RS
31 Januari 2023.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa