Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri sita za Mkoa wa Simiyu zimetoa shilingi 138,030,500/= kwa vikundi 122 vya wanawake kama mikopo kutoka katika asilimia nne ya mapato ya ndani ya halmashauri, kwa ajili ya kuwapatia mitaji ya kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa naiba yake na Mwanasheria wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bi, Manahamisi Kawega wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani Machi 08, 2021 ambayo kimkoa yamefanyika Wilayani Maswa.
“Halmashauri ya Mji wa Bariadi, imetoa shilingi 10,000,000/= kwa vikundi 25, Halmashauri wilaya ya Bariadi shilingi 48,000,000/= vikundi 37, Busega shilingi 16,000,000/=kwa vikundi 16, Itilima shilingi 12,000,000/= vikundi 12, Maswa shilingi 39,200,000/= vikundi 18 na Meatu shilingi 12,830,500 kwa vikundi 14,” alisema.
Aidha, Mmbaga amewaagiza Wakurugenzi wa Mamalaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutenga na kupeleka fedha asilimia nne kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake kwani haina riba kuliko mikopo kutoka taasisi nyingine za kifedha.
Vile vile Mmbaga amesema kauli mbiu ya siku ya wanawake mwaka 2021 “ Wanawake katika Uongozi:Chachu ya kufikia Dunia yenye Usawa” itumike kuwawezesha wanawake kwenye nafasi za uongozi katika mkoa wa Simiyu kwa kuwa jamii bado haijatambua umuhimu wa kumuwezesha mwanamke nafasi za uongozi tunapoelekea kwenye Dunia ya usawa.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Bi. Haula Kachwamba ametoa wito kwa viongozi wanawake kufanya kazi kulingana na matarajio ya wanawake huku akisisitiza wahakikishe wanatafuta ufumbuzi wa changamoto za wanawake.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera amewataka wanawake kujiamini na kujitokeza katika fursa mbalimbali za uongozi katika jamii kwa kuwa viongozi wanawake ni wachache, hivyo kila fursa inapopatikana wasisite kujitokeza ili kuwe na viongozi wengi wanawake katika kuelekea dunia yenye usawa.
Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani Kimkoa yaliambatana na maonesho ya shughuli za wanawake wajasiriamali, uchangiaji damu, kutoa misaada kwa wagonjwa ambapo chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali (TUGHE) walitoa msaada wa mashuka 30 kwenye wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2021/03/zaidi-ya-milioni-138-zatolewa-mikopo.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa