Shirika lisilo la kiserikali la World Vision limekabidhi msaada wa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona pamoja na Jengo la zahanati kwa uongozi wa mkoa wa Simiyu vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 95.7.
Akikabidhi msaada huo jana Mei 08, 2020 kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini katika kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa, Meneja wa World Vision Kanda ya Ziwa, Bw. John Massenza amesema pamoja na zahanati wamekabidhi mipira ya kuvaa mikononi, vitakasa mikono,vipaza sauti, barako na mavazi maalum ya wataalam wa afya.
"Pamoja na zahanati leo tunakabidhi mipira ya kuvaa mikononi boksi 500,vitakasa mikono lita 200,vipaza sauti 26 kwa wahudumu wa afya ngazi za jamii na mavazi ya kujikinga na maambukizi 60 na barakoa aina ya N95, vyote vikiwa na thamani ya shilingi 95,755,000/=, "alisema Massenza.
Aidha, ameongeza kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na ofisi ya mganga mkuu wa mkoa wa Simiyu na waganga wakuu wa wilaya litaendelea kutoa misaada ya vifaa , vitendea kazi, kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na kuhakikisha wanasambaza elimu ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID 19) inayosababishwa na virusi vya Corona. .
" Shirika limeendelea kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya mapafu kwa njia ya matangazo na tumewezesha mafunzo kwenye makundi tofauti ya watu ambayo yatasambaza elimu hii kwa jamii mfano wa makundi hayo ni viongozi wa dini,wahudumu wa afya ,viongozi wa serikali, "alisema Massenza.
Akipokea vifaa hivyo pamoja na zahanati Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw Jumanne Sagini ameishukuru World Vision kwa msaada huo ambao umetolewa kwa Halmashauri zote sita pamoja na kuwa shirika hilo linafanya kazi na halmashauri ya wilaya ya Maswa na Itilima; huku akibainisha kuwa vifaa kinga hivyo vitawajengea ujasiri watoa huduma za afya kuwahudumia watakaobainika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Naye mganga mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt.Festo Dugange amesema wamekuwa wakitekeleza afua mbalimbali za kuhakikisha wananchi wanakuwa salama dhidi ya ugonjwa wa COVID 19 kwa kutoa elimu ya namna ya kujikinga, huku akiongeza kuwa mkoa upo vizuri na tayari umeshatenga vituo endapo watapatikana washukiwa wa ugonjwa huo.
Akiongea kwa niaba ya wakurugenzi wa halmashauri mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Dkt. Frederick Sagamiko amelishukuru shirika hilo kwa kuwa msaada mkubwa kwenye shughuli za maendeleo mkoani hapo hususani katika wilaya ya Itilima na Maswa ambapo kwa Maswa mbali na kuwajengea zahanati pia limesaidia katika ujenzi wa kiwanda cha viazi lishe na wilaya ya Itilima kiwanda cha sabuni.
Kwa upande wao wananchi wa kijiji cha Wigelekelo wakiwemo Mbuke Kemakema na Mashauri Ngeme wamelipongeza shirika hilo kwa ujenzi wa zahanati ambayo itawasaidia kupata huduma za afya karibu kwani awali walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA LINKI HII:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/05/world-vision-yakabidhi-vifaa-vya.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa