Waziri wa mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina amewaongoza wakazi wa Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu katika mazishi ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mwanhuzi wilayani Meatu Elias Shukia aliyefariki katika ajali ya gari Mkoani Singida akitokea Dodoma na kusababisha kifo chake na dereva na kusababisha watu wengine watano kujeruhiwa.
Ajali hiyo imetokea Julai 14 eneo la Mkiwa Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida ,baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina Toyota landcluser DFPA 0148 la Halmashauri ya Meatu kupasuka tairi na kupinduka mara tatu na kusababisha vifo hivyo viwili,huku majeruhi wa ajali hiyo Mkurugenzi Mtendaji, Mwenyekiti wa Halmashauri na Maafisa wa Halmashauri hiyo walipata majeruhi.
Mpina ametoa pole kwa familia, wananchi, Chama Cha Mapinduzi na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu na kuwataka kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa kuondokewa na madiwani watatu na dereva katika matukio mawili tofauti ya ajali na akawaomba wasifikiri kitu kingine tofauti juu ya kutokea kwa ajali hizo badala yake wajue kuwa ni mapenzi ya Mungu.
“ Kuna watu wanaweza wasiamini kuwa ajali zinaweza zikatokea Meatu kwa muda fupi hivi kama ilivyotokea kwetu, naomba ndugu zangu wananchi, viongozi tusiingie kwenye mtego huo tujue tu kuwa haya ni mapenzi ya Mungu kama walivyosema viongozi wetu wa dini kuwa Mungu ndiye anayejua hatma ya maisha yetu” alisema Mpina.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa pole kwa familia, chama na wananchi kwa msiba huo na amewaagiza Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kuhakikisha stahili zote za marehemu zinalipwa kwa wakati kwa familia ya marehemu.
Aidha, amewaomba viongozi wa dini kufanya maombi kwa ajili ya wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kuomba Mwenyezi Mungu kuwaepusha viongozi na wananchi na mitihani ya ajali iliyotokea mfululizo.
“Wakati tunawaaga madiwani wetu wale wawili waliofariki kwenye ajali ya kwanza, Mwenyekiti wa Halmashauri na madiwani wengine walikuwa kwenye matibabu kwa sababu ya ajali, leo tunamuaga Mhe. Shukia Mkurugezi na Mwenyekiti wako kwenye matibabu kwa sababu ya majeraha waliyoyapata katika ajali, sisi kama wanadamu tunaamini kwenye ulimwengu wa roho tuna nafasi ya kuomba, niwaombe viongozi wa dini tumwombe Mungu atuepushe na mitihani hii” alisema
Mbunge wa Jimbo la Meatu Salum Khamis amesema kifo cha mhe. Shukia ni pigo kubwa kwa kata ya Mwanhuzi na Meatu kwa ujumla kwa kuwa marehemu Shukia enzi za uhai wake alikuwa mtetezi ndani ya Chama Cha Mapinduzi na wananchi katika shughuli za maendeleo.
Akitoa mahubiri wakati wa ibada ya Mazishi, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Dkt. Emmanuel Makala aliwakumbusha waombolezaji wote kuishi wakimtegemea Mungu, kwa kuwa kila mtu hapa duniani anaishi kwa neema ya Mwenyezi Mungu, hivyo wanapaswa kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.
Marehemu Shukia ameacha mke na watoto wanne, BWANA ALITOA , BWANA AMETWAA JINA LA BWANA LIHIMIDIWE. AMINA!
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/07/waziri-wa-mifugo-aongoza-waombolezaji.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa