Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameagiza Wakala wa Majengo nchini TBA kurejesha fedha ilizokabidhiwa na wizara yake kwenye ofisi za TBA mjini Bariadi ili zitumike kukamilisha mradi wa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Simiyu ambao kasi ya ujenzi wake kwa sasa hairidhishi.
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo katika ziara yake ya siku moja mjini Bariadi, mkoani Simiyu kukagua ujenzi wa jengo litakalotumika kutoa huduma za maabara, upasuaji na mionzi na kusema kuwa serikali imejiwekea malengo ifikapo Julai Mosi wananchi waanze kupata huduma kwani tayari fedha zote za mradi huo zimekwishalipwa.
“Wizara tayari imeshalipa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa TBA lakini cha ajabu wao wameleta shilingi milioni 430 tu, na matokeo yake ndio haya, ukiangalia muda tuliopewa kukamilisha kazi hii si rafiki, sasa ninawaagiza TBA walete hiyo pesa site ili kazi iendelee”.
“ Hivi jamani kwa kasi hii kweli tunaweza kuendelea kuweka matumaini kwa hawa ndugu zetu, ukiangalia mheshimiwa Rais ametupatia shilingi bilioni 2.5 tujenge jengo la mama na mtoto sasa kwa utaratibu huu wa kusuasua mnadhani tutafika kweli, mimi nadhani umefika wakati tutumie force account kwenye mradi huu, Bariadi kuna mafundi wengi wazawa wenye uwezo mkubwa wa kutufanyia kazi hii”, alisisitiza Waziri Ummy.
Kuhusu mpango wa serikali wa kuboresha huduma za rufaa katika hospitali zote za mkoa nchini, Waziri Ummy amesema wizara imedaa utaratibu ambapo kila hospitali itapata madaktari bingwa 16 katika fani 8 yaani madaktari 2 kila fani wakiwemo madaktari bingwa wa akina mama, watoto, Mishipa ya fahamu, mifupa, njia ya mkojo, dawa za usingizi na mionzi.
“ Tunataka tuwe na maabara kubwa za kisasa pamoja na jengo la mionzi kama tunalojenga hapa Simiyu katika kila hospitali ya rufaa ya mkoa, tunamshukuru sana mheshimiwa rais kwa kutupatia shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo uchunguzi, ninaomba kila mmoja wenu kwa nafasi yake ahakikishe miradi yote inayotumia fedha za serikali inatekelezwa kwa ufanisi”, aliongeza Waziri Ummy.
Akijibu maombi ya viongozi wa chama na serikali wa mkoa wa Simiyu kuhusu tatizo la usafiri kwa watumishi watakaopangiwa kufanya kazi katika hospitali ya rufaa ambayo kwa sasa haina nyumba za watumishi, Waziri Ummy amewahakikishia kuwa Wizara itaangalia uwezekano wa kuipatia hospitali hiyo basi maalumu la watumishi halikadhalika itaweka bajeti ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika mwaka wa fedha ujao.
Akiwa katika hospitali ya wilaya ya Bariadi ya Somanda, Waziri Ummy alielezea kutoridhiswa na utaratibu wa kutoa huduma katika wodi ya wazazi na kumwagiza mganga mkuu wa mkoa kuzifanyia marekebisho kasoro zote zilizobainika ili huduma zinazotolewa ziendane ni miongozo ya wizara.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amemhakikishia Waziri Ummy kuwa, mkoa utasimamia kikamilifu utakelezaji wa mradi huo na kusisitiza kuwa pale ambapo pamebainika kuwa na dosari atahakikisha zinarekebishwa ili kuongeza ufanisi katika mradi huo.
“Mhe Waziri mimi nina amini kukamilika kwa hospitali hii ni mkombozi kwa maelfu ya wananchi wetu wa mkoa wa Simiyu, sasa wajiandae kupata huduma bora zikiwemo za bima ya afya ambazo zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa, kwa ujumla tunaamini zitawahamasisha watu wengi zaidi kujiunga na huduma hiyo”, alisisitiza RC Mtaka.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amekamilisha ziara yake mkoani Simiyu na Kuelekea katika mikoa ya Geita na Shinyanga.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa