Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la viwanda vidogo nchini SIDO kuweka mikakati ya kupanua wigo wa shughuli zake kwa kuanzisha vituo katika ngazi ya halmashauri za wilaya ili kuwafikia wajasiliamali wengi zaidi, kuwajengea uwezo, kuwapa miongozo bora ya namna ya kuendesha shughuli zao kwa tija na kuwaunganisha na taasisi za fedha waweze kupata mikopo.
Waziri mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo katika ufunguzi wa maonesho ya SIDO Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Nyakabindi Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu ambapo amesema umefika wakati kwa SIDO kutilia mkazo sekta ya viwanda na hivyo kuifanya jukwaa la kuwakutanisha wabunifu pia kuwapa fursa ya kuonyesha uwezo wao katika matumizi ya teknolojia rafiki na rahisi zitakazoharakisha maendeleo ya viwanda nchini.
Pia Waziri Mkuu Majaliwa amesema SIDO inapaswa kujielekeza katika kubuni mashine , mitambo na teknolojia rahisi zitakazotumika kuongeza thamani ya bidhaa na kusisitiza kuwa kutokana na umuhimu wa sekta ya viwanda nchini katika kukuza ajira na kuongeza pato la taifa serikali itaendelea kuweka miundombinu wezeshi itakayoharakisha kasi ya ukuaji wa viwanda.
“ Bila shaka nyote mnafahamu tumedhamiria kufikia uchumi wa kati kufikia mwaka 2025, ninaamini tunao uwezo wa kulifikia lengo hili, sasa tunachotakiwa kufanya kuhakikisha halmashauri zetu zote zinatenga maeneo maalumu kwa ajili shughuli za viwanda kama mlivyofanya hapa Simiyu, lakini pia lazima mhakikishe mnawajengea uwezo wajasiliamali ili waweze kuingia katika soko la ushindani, alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa”.
Waziri Mkuu Majaliwa amewasisitiza SIDO waendelee kubuni mikakati itakayoleta mabadiliko katika sekta ya viwanda huku akiwataka wananchi kuthamini bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini ambazo tayari zimeonyesha kukidhi mahitaji ya soko.
Halikadhalika waziri Mkuu Majaliwa ameziagiza halmashauri za wilaya nchini kuendelea kutekeleza agizo la kutenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanaweke, vijana na walemavu huku akiwasisitiza madiwani katika halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa agizo hilo.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa ameupongeza uongozi wa mkoa wa Simiyu kwa kujenga mahusiano mema na wananchi, viongozi wa kisiasa pamoja na taasisi mbalimbali jambo ambalo amesema ni chachu ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani Simiyu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo(SIDO), Prof. Sylvester Mpanduji amesema Shirika hilo litaendelea kutoa mafunzo kwa wajasriamali ili kuwajengea uwezo zaidi, ambapo amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 SIDO imetoa mafunzo kwa wajasiriamali 16,900.
Aidha, Prof. Mpanduji ameishukuru Serikali kwa kutenga shilingi bilioni 29 katika mwaka wa fedha 2018/2019 ambazo zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali za wajasiriamali ikiwemo upatikanaji wa mashine mpya zitakazotumika katika vituo vya SIDO vya kuendeleza viwanda, kukopesha wajasiriamali mitaji na kujenga miuondombinu mingi ya viwanda katika sehemu hapa nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amemhakikishia Waziri mkuu kuwa Mkoa huo utahakikisha unaendelea kutekeleza maagizo ya serikali ikiwemo agenda ya kitaifa ya Uchumi wa Viwanda kupitia Falsafa ya Wilaya Moja Bidhaa Moja.
“Simiyu ni Mkoa wenye ajenda na kazi yetu ni kutekeleza maelekezo na miongozo yote ya Serikali, tunatekeleza Sera ya Viwanda chini ya Falsafa ya Wilaya Moja Bidhaa Moja na sasa tunaenda kwenye utekelezaji wa Kijiji Kimoja Bidhaa Moja na sisi tunaamini Mapinduzi ya Viwanda yanaanza na SIDO” alisema Mtaka.
Maonesho hayo ya SIDO ambayo yanafanyika kwa mara ya kwanza mkoani Simiyu yamehudhuriwa na wajasiliamali zaidi ya 500 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini ambayo yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 28, 2018.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI FUGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/10/waziri-mkuu-majaliwa-aitaka-sido.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa