Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (Mb) amewataka wakazi wa Lamadi wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, kurasimisha makazi yao katika kipindi hiki ambacho zoezi la urasimishaji makazi kwa gharama nafuu linaloendelea wilayani humo.
Waziri Lukuvi ametoa wito huo leo wakati wa zoezi la kuhamasisha urasimishaji makazi yalioendelezwa kiholela na kukabidhi hati miliki 122 kwa wananchi wenye maeneo yaliyorasimishwa katika Kijiji cha Lamadi.
Lukuvi amesema Lamadi ni Mji wa Kibiashara hivyo wakazi wake wanapaswa kujenga nyumba zao katika maeneo yaliyopimwa na kutolewa hati ili waishi katika makazi rasmi na salama.
“Mhe.Rais mpendwa wenu ametuagiza kuja Lamadi kurasimisha makazi yaliyokuwa holela ili yawe makazi salama na rasmi, huu ni upendeleo maalum ametoa kwamba waliojenga katika maeneo haya yanayoitwa makazi holela wengi ni maskini na siyo makosa yao, inawezekana wakati wanajenga hakukukwa na viwanja vilivyopangwa na kupimwa na Serikali” alisema
“Mhe.Rais ameagiza watu wote wanaotaka kushiriki zoezi hili wachangamkie fursa hii, ametoa ofa kuwa ninyi ambao mlijenga siku nyingi na mnataka kuongeza thamani ya nyumba zenu mtoke kwenye mtaji mfu na kufanya majengo yenu yatumike kama mtaji wa maendeleo” alisisitiza.
Lukuvi amesema wananchi watakaporasimisha maeneo yao watapata fursa ya kutumia hati miliki zao kupata dhamana ya mikopo katika benki mbalimbali kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi.
Aidha, amesema ofa hii ya kurasimisha maeneo ni ya muda tu, hivyo akawataka wakazi zaidi ya 5000 waliopimiwa viwanja vyao kulipia kabla ya tarehe 30 Juni 2017 ili waweze kupewa hati miliki za maeneo yao na ambao bado hawajapimiwa waone umuhimu wa kupima na kulipia viwanja vyao pia kabla ya muda huo.
Amesema wananchi wanapaswa kusaidiana na Uongozi wa Wilaya ya Busega katika kufanikisha zoezi la urasimishaji kwa kuchangia gharama kidogo ili wapimiwe, warasimishiwe, wawekewe alama za mipaka, wapewe ramani na kupewa hatimiliki za maeneo yao na akawataka pia kurasimisha maeneo ya mashamba na kuyatafutia hati.
Wakati huo huo Mhe.Lukuvi amewataka wananchi wote waliopata hati na wale watakaendelea kupewa kulipa kodi ya ardhi ya kila mwaka kwa Serikali na wale watakaokaidi kulipa kodi hiyo hati zao zitafutwa.
Akizungumza baada ya kupokea hati kutoka kwa Waziri Lukuvi, Mzee Musa Metusela Kole mkazi wa Lamadi, ameishukuru Serikali kwa kurasimisha maeneo yao kwa gharama nafuu na huduma nzuri kutoka kwa wataalam ambao waliwafuata wananchi katika maeneo yao na akatoa wito kwa wananchi wengine kurasimisha maeneo yao ya makazi na mashamba pia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Ndg.Anderson Njiginya amesema zoezi la urasimishaji ardhi kwa wakazi wa Lamadi limechangia kuongeza mapato yatokanayo na ardhi kwa Serikali, kupunguza migogoro ya ardhi baada ya kupima na kuweka mipaka ya kudumu katika viwanja na kuwawezesha wananchi kutumia hati za maeneo yao kwa shughuli zao za kiuchumi.
Zoezi la urasimishaji wa makazi katika Kituo cha Kibiashara Lamadi lilianza Mwezi Julai 2016 hadi sasa ambapo shughuli ya utambuzi wa miliki umekamilika kwa kupata viwanja 5223 na shughuli ya umilikishaji Viwanja ilianza Aprili 11, 2017 ambapo hadi sasa hati 138 zimeandaliwa kati ya hizo 122 zimekabidhiwa leo kwa wamiliki na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (Mb).
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa