Waziri wa nishati Dkt Medard Kalemani amemuondoa Meneja wa TANESCO wilaya ya Meatu mkoani Simiyu Bw.Amos Mtae katika nafasi ya umeneja baada ya kushindwa kusimamia usambazaji wa umeme kupitia Mradi wa Umeme vijijini (REA) wilayani humo na amemwagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kumpangia kazi nyingine.
Waziri KALEMANI amechukua hatua hiyo katika mkutano wa hadhara mjini Meatu akiwa katika ziara yake ya kukagua kazi zinazofanywa na wakandarasi wa mradi wa Umeme vijijini REA awamu ya tatu Septemba 20, 2018, ambapo anaanzia katika uzinduzi wa mradi wa umeme katika ofisi ya kijiji cha Dakama wilaya ya Meatu.
Dkt. Kalemani ameoneshwa kutoridhishwa na kasi ya mkandarasi anayesambaza umeme wilayani Meatu ambaye ni kampuni ya White City, kutokana na kutokuonekana katika vituo na kutokuwa na vifaa vya kutosha na vituo vya kutosha.
“Kasi ya mkandarasi hapa ni mbovu niliteegemea nione wakandarasai wanachakarika maana kote nilikotoka nimekuta wanachakarika, pili nilitegemea nione yadi ya vifaa vya wakandarasi wetu”
“Huyu meneja ndiye msimamizi wa wakandarasi, namuuliza anasema hajui leo wakandarasi wako wapi sasa anasimamia nini? Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO pokea maelekezo, kuanzia sasa huyu Meneja wa TANESCO Wilaya mtoe, weka Meneja mwingine kuanzia kesho hapa, wananchi wanataka umeme hapa” alisema Dkt. Kalemani.
Katika hatua nyingine Dkt. Kalemani amewahakikishia wananchi wa vijiji 36 vya wilaya ya MEATU kupata umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya tatu na akawasisitiza kuwa umeme utakapowafikia wautumie kwa ajili ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa wa Simiyu una asilimia sabini ya Mradi wa Umeme wa REA ambapo wilaya ya Meatu ilikuwa nyuma katika mradi huo ikilinganishwa na wilaya nyingine.
Aidha, amesema wananchi wa Meatu wakipata umeme utekelezaji wa Sera ya Viwanda utafanikiwa kwa kuwa wilaya hiyo ndiyo wilaya inayoongoza kwa kilimo cha pamba Tanzania na ndiyo wilaya inayoongoza kwa kilimo cha alizeti katika mkoa wa Simiyu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Meatu Mhe. Salum Khamis akizungumza kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo hilo ameishukuru Serikali kwa kufanikisha utekelezaji wa usambazaji wa umeme katika vijiji vya wilaya hiyo na akaomba Wakandarasi waongeze kasi ili umeme awafikie wananchi kwa wakati
Naye mwakilishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Barnabas Lupande ameahidi kuyafanyia kazi maagizo ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani aliyoyatoa katika kuakikisha kazi kusambaza umeme kwa wananchi inafanyika inavyotakiwa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/09/waziri-kalemani-amuondoa-meneja-wa_20.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa