Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki ametoa wito kwa chama cha wanataaluma na wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania (ATAPE) na wawekezaji wengine wazawa kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini na kusajili miradi yao ya Uwekezaji katika Tume ya uwekezaji ya Taifa (TIC).
Kairuki ameyasema hayo wakati akifunga Mkutano wa 20 wa chama cha wanataaluma na wajasiriamali wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania (ATAPE) Mjini Bariadi, ambapo amebainisha kuwa kwa mwaka huu 2019 wawekezaji wazawa zaidi ya asilimia 72 wamesajili miradi yao ya uwekezaji TIC.
“ Kwa mwaka huu peke yake tumepata wawekezaji wazawa waliosajili miradi yao ya uwekezaji TIC zaidi ya asilimia 72, hii inanipa faraja sana kama waziri wa nchi ninayesimamia uwekezaji ninapoona Watanzania wenzangu wanachangamkia fursa”
"Naomba mchangamkie fursa hizo kwa sababu wawekezaji wa nje tunapenda waje tu endapo watakuja kuungana nasi kwenye mtaji, kubadilishana nasi ujuzi na uzoefu " alisema Kairuki.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji na kuweka vipaumbele kwa ajili ya kuvutia wawekezaji katika sekta ambazo zitakuwana athari na tija kubwa kiuchumi kwa wananchi, ili kuimarisha minyororo ya thamani katika kilimo,uvuvi, na mifugo ambayo ni maeneo yanayoajiri Watanzania wengi zaidi.
Aidha, Waziri Kairuki amezitaja sekta nyingine za kipaumbele kuwa ni uzalishaji wa mafuta ya kula kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini, uzalishaji wa sukari, uzalishaji wa dawa za binadamu, vifaa tiba na kemikali, ujenzi wa miundombinu ya uvuvi wa kisasa, viwanda vya kuchakata samaki, kusindika nyama, viwanda vya kubangua korosho, viwanda vitakavyotumia pamba na viwanda vya pembejeo na mbolea.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ameipongeza ATAPE kwa jinsi inavyoshirikiana na Serikali katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo sekta ya afya, elimu, maji pamoja na huduma nyingine.
Kairuki amesema serikali pekee haiwezi kutatua changamoto zote hivyo kwa kushirikiana na wadau ikiwemo taasisi za dini wanaweza kuwahudumia wananchi na kuleta mabadiliko chanya ikiwa ni pamoja na kuhubiri amani, huku akisisitiza kuwa masomo ya ujasiriamali yanayotolewa kwa wana ATAPE wayatumie kwa manufaa ya kanisa na jamii kwa ujumla.
Awali akimkatibisha waziri Kairuki, mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkutano huo umewasaidia watu wa Simiyu kukutana na watu wa maeneo mengine hatua iliyopelekea kubadilishana uzoefu sambamba na kuongeza na kupata masoko mapya .
‘’watu wetu wameongeza wigo wa masoko, mmebadilishana uzoefu ....huu ni mkoa wa kibiashara na ni mkoa wenye fursa nyingi; tunajenga tawi la chuo cha usimamizi wa fedha (IFM) hivyo ninawaalika wafanyabiashara na Watanzania wote kuja kuwekeza ujenzi wa hosteli eneo lile linalojengwa tawi hilo"alisisitiza Mtaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ATAPE Freddie Manento amesema kwa miaka mitatu ATAPE imewekeza miradi ya bilioni 1.2 katika miradi yenye manufaa kwa kanisa, wanajamii na wana ATAPE.
Alisema wamewekeza kwenye miradi ya maji kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa, miradi ya miti ya matund), korosho na miradi ya mashamba ya mihogo kwa kutengeneza ajira na faida katika vijiji walivyolima mashamba yao.
‘’Wana ATAPE wamejitoa kwelikweli na wameitikia dhana yetu ya kutumia vipaji na rasilimali zetu kwa ajili ya kazi ya MUNGU, hii iko katika mathayo 28;19, 20…hii ndio dhana yao’’ alisema Manento.
Mkutano wa Wanataaluma na Wajasiriamali (ATAPE) kutoka kanisa la Waadventista Wasabato umefanyika mkoani Simiyu kwa muda wa siku sita ambapo umehudhuriwa na wananchama zaidi ya 1500.
.....MWISHO....
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:https://simiyuregion.blogspot.com/2019/04/waziri-kairuki-atoa-wito-kwa-wawekezaji.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa