Waziri wa Madini Angela Kairuki amemwaagiza Mkandarasi anayejenga Kituo cha umahiri cha Madini mkoani SIMIYU, Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) kukamilisha ujenzi ifikapo Januari 2019, ili kiweze kuwasaidia wachimbaji Katika masuala mbalimbali ikiwa ni kupata mafunzo ya uchimbaji wenye tija.
Kairuki ametoa agizo hilo alipotembelea na kuona hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Kituo hicho unaoendelea katika eneo la Nyaumata makao makuu ya mkoa wa SIMIYU Mjini Bariadi, Novemba 22, 2018.
Kairuki amesisitiza usimamizi uimarishwe zaidi na fedha ziweze kutolewa kwa wakati ili jengo hilo liishe katika muda uliopangwa, huku akiupongeza uongozi wa mkoa wa SIMIYU kwa kukubali kutenga eneo la ujenzi wa kituo hicho.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki amesema Wizara ya madini itahakikisha inawasadia wachimbaji wa chumvi mkoani Simiyu ili chumvi inayozalishwa iweze kuwa bora na yenye uwezo wa kushindana katika soko, huku akiwakumbusha wenye leseni za Madini kuzitumia.
“ Kama Wizara tutashirikina na mkoa wa Simiyu katika kuhakikisha wachimbaji wanachimba kwa tija lakini pia kuleta migodi ya mifano na namna za nyingine ya uchenjuaji, pia ikiwemo na hiyo chumvi, ambayo tutahitaji izalishwe katika ubora, ushindani na kuwekwa katika vifungashio bora”
“Tuendelee kuhamasisha wachimbaji wengi zaidi kuendelea kuchimba wasishikilie tu leseni,tunataka kuona ule msamaha uliotolewa na Mhe. Rais kutoka tozo 16 hadi kufikia tozo 09 kwenye chumvi uwe na faida kwao” alisema Waziri Kairuki.
.
Kwa upande wake Mkurugenzi mwendeshaji kutoka SUMA JKT, Mhandisi Morgan Nyonyi amesema watatekeleza maelekezo ya Mhe.Waziri na kubainisha kuwa hadi sasa ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 35, kufikia Januari 22, 2019 litakuwa limekamilika na mpaka kukamilika kwa litagharimu takribani shilingi bilioni 1.3.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka uwepo wa kituo cha Umahiri Mkoani hapa utasaidia kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo na wakubwa wa chumvi katika Wilaya ya Meatu, pamoja na wazalishaji wengine kwa ujumla ambao watajikita katika utengenezaji wa chumvi hali itakayosaidia wananchi Simiyu na maeneo mengine nchini kutumia chumvi itakayozalishwa Meatu badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.
Ameongeza kuwa upembuzi yakinifu juu ya uanzishwaji wa kiwanda cha kutengeneza chumvi wilayani Meatu umeshafanyiwa upembuzi yakinifu na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kijamii na Kiuchumi (ESRF) na unatarajiwa kuwa mradi mwingine mkubwa wa Wilaya hiyo baada ya mradi wa kiwanda cha kusindika maziwa.
Aidha, amesema kukamilika kwa kituo hicho kutachangia kutoa mwanya na fursa kwa wananchi wa Simiyu kuwa na uwekezaji mwingine(madini) zaidi ya kilimo na mifugo, huku akibainisha kuwa kitachangia pia kukaribisha wawekezaji wengi kutokana na kuwepo kwa uhakika wa mahali pa kupata mafunzo na kupima sampuli mbalimba za madini .
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU TUKIO HILI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa