Waziri wa nchi ,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo ametoa agizo kuwa ifikapo Julai 30, 2019 hospitali zote za wilaya zinazojengwa nchini ziwe zimekamilika .
Jafo ameyasema hayo akiwa kwenye ziara ya siku moja mkoani Simiyu ambapo alitembelea miradi mbalimbali ukiwemo wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Itilima,. ujenzi wa barabara ,ujenzi wa kiwanda cha chaki na ujenzi wa kituo cha mabasi(stendi) cha kisasa, huku akipongeza ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Itilima kwa kizingatia viwango, mahitaji na ubora katika ujenzi.
Aidha amesema kuwa hakuna sababu za fedha kuongezwa kiasi kilichotolewa awali kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba ya awali kinatosha kukamilisha huku akitolea mifano ya hospitali ambazo zimeshakamilika kwa kiasi hicho kilichotolewa awali.
Akiwa wilaya za Meatu na Maswa waziri Jafo amekagua na kuridhishwa na ujenzi wa barabara zilizojengwa na mkandarasi CHICO kwa kiwango cha lami ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli aliyoitoa akiwa ziarani mkoani hapo zenye urefu wa kilometa tatu( kilometa moja na nusu kwa kila wilaya)
“Nikupongeze sana mratibu wa TARURA Mhandisi Dkt Philimon Msomba kwa kazi hii nzuri kikubwa wananchi muutunze mradi huu ,kwanza nimefarijika sana kukuta hadi taa za barabarani zipo hongereni sana ”alisema waziri Jafo.
Kwa upande wake Mbunge wa Maswa Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini Mhe.Stanslaus Nyongo amemuomba Waziri Jafo kabla mkandarasi hajaondoa vifaa vyake eneo la ujenzi wa barabara ni bora ukafanyika mchakato wa kuongeza kiasi kingine cha pesa kwa ajili ya kilometa 1.5 zilizobaki.
Katika hatua nyingine akiwa Mjini Bariadi Waziri Jafo ameridhishwa na ujenzi wa kituo cha mabasi kinajengwa Mjini hapo na kumtaka mkandarasi Kampuni ya Halem and Kings Builders Co Ltd kutoka Dar es salaam kukamilisha ujenzi ifikapo Septemba 2, 2019 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 87 na mpaka kukamilika kwake ujenzi utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 7.2
Pamoja na hayo waziri Jafo alitembelea ujenzi wa kiwanda cha chaki na kiwanda cha vifungashio unaoendelea wilayani Maswa na kupata taarifa ya ujenzi huo ambao ulipaswa kukamilika Augost 7 lakini mkandarasi SUMA JKT kaomba kuongezewa muda hadi sept 22 ,2019 kwa kile alichodai awali walipata changamoto zilizopelekea kuchelewa kuanza .
“kwenye taarifa yenu ujenzi huu ulipaswa kukamilika lakini hapa mnasema muongezewe muda ,mradi una lengo maalum na mkakati kiwanda kikamilike kianze kutoa products(bidhaa), mimi niwahakikishie ntakuja hapa tarehe 22 au 23 kujihakikishia kama kweli ujenzi huo umekamilika ” alisema waziri Jafo
Wakiongea kwa niaba ya wananchi Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinguzi (CCM) wilaya ya Maswa Mhandisi. Paul Jidayi na Mkuu wa Wilaya ya Meatu Dkt. Joseph Chilongani wameishukuru Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza ahadi ya Mhe. Rais na kubainisha kuwa watashirikiana na wananchi kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo inatunzwa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/07/waziri-jafo-aagiza-hospitali-za-wilaya.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa