Wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III wametakiwa kubuni miradi midogo midogo kwa kutumia fedha wanazopata ili kujiongezea kipato.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini wakati wa ziara yake wilayani Itilima ya kukagua visima vya maji ambavyo ni miongoni mwa miradi ya kutoa ajira za muda kwa walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya Maskini TASAF III.
Sagini amesema wanufaika wa TASAF ikiwa ni pamoja na waliopata ajira za muda katika uchimbaji wa Visima na kulipwa ujira kidogo watumie fedha hizo kujikimu na kuanzisha miradi midogo midogo ikiwemo ya biashara ndogo ndogo na ufugaji wa kuku, bata, mbuzi na kondoo.
“ Mradi huu hautadumu milele nawashauri katika kidogo mnachokipata mkitumie vizuri, anzisheni miradi midogo midogo itakayowasaidia kuboresha kipato katika kaya zenu, wenye uwezo wa kufuga wafuge, wenye uwezo wa kufanya biashara ndogo ndogo wafanye”
Mwenyekiti wa kijiji cha Nanga Dismas Lyang’ombe amesema baadhi ya wanufaika wa mradi wa TASAF waliohusika katika ujenzi wa visima vinne vilivyojengwa na Serikali kupitia Mradi wa TASAF kwa kushirikiana na wananchi na kupewa ujira wa shilingi 2300 kwa siku, wameonesha mabadiliko katika kaya zao tofauti na ilivyokuwa awali, ikiwa ni pamoja na kufuga kuku, mbuzi na kuezeka nyumba zao kwa bati.
Aidha, Lyang’ombe ameishukuru Serikali kwa kujenga visima hivyo kwa kuwa vimewasaidia wananchi wake kupata huduma ya maji katika umbali mfupi
Kwa upande wao wananchi wa vijiji vya Nguno, Nanga na Laini B vyote vya Wilaya ya Itilima alivyovitembelea Katibu Tawala Mkoa Simiyu, wameomba Serikali hiyo kutibu maji yanayopatikana katika visima hivyo ili wapate maji safi na salama.
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Ndg. Mariano Mwanyigu amesema Halmashauri yake itaandaa utaratibu mzuri wa kitaalam kupitia wahandisi wa maji kuhakikisha maji yanatibiwa na wananchi wanapata maji safi na salama.
Miradi ya ajira za muda kwa wanufaika wa Mradi wa TASAF hutekelezwa katika kipindi kigumu kiuchumi ili kuwasiadia wanufaika hao na katika wilaya ya Itilima imeanza kutekelezwa mwezi Disemba 2016 hadi Machi 2017.
Jumla ya miradi 161 imeibuliwa katika vijiji 65 vilivyo kwenye mpamgo, katika kipindi cha kwanza cha utekelezaji wa miradi ya kutoa ujira ni visima 161 vinavyotakiwa kukamilishwa na visima 95 vimekamilika vinatoa maji, 66 viko katika hatua ya kufunikwa na vinatoa maji.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa