Wananchi wa Vijiji vya Igegu na Ng’arita Kata ya Sapiwi wilayani Bariadi wameridhia kuachia maeneo yao kupisha Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Mkoani Simiyu ambacho kinatarajiwa kujengwa katika eneo la Igegu wilayani Bariadi.
Wananchi hao wameyasema hayo Septemba 14, 2018 wakati wa uzinduzi wa zoezi la Uthamini na upimaji wa maeneo hayo, ambalo linatarajiwa kumalizika baada ya mwezi mmoja na wiki mbili kuanzia sasa.
Wamesema kuwa wamefurahishwa na hatua ya Serikali kujenga Kiwanja cha Ndege wilayani Bariadi na kwa kuwa ujenzi huo ni suala la maendeleo hawawezi kupinga, huku wakiiomba Serikali kuhakikisha wanalipa fedha za fidia kwa wakati mara tu baada ya kukamilisha zoezi la uthamini na upimaji wa maeneo hayo.
“Kwa kuwa ujenzi wa kiwanja cha ndege ni maendeleo hatuwezi kukataa kutoa maeneo yetu, tumekubali kutoa maeneo ila ombi letu kwa Serikali tunaomba tulipwe fidia ya maeneo yetu kwa wakati na tulipwe kwa haki” alisema Ndaturu Malemi mkazi wa Kijiji cha Igegu.
“Tumekubali kutoa maeneo yetu Uwanja wa Ndege ujengwe, ushauri wangu tu ni kwamba kwa kuwa tunaelekea msimu wa kuandaa mashamba baada ya tathmini tunaomba tuliokuwa na maeneo hapa tuambiwe mapema kama ujenzi utaanza au tunaweza kuendelea na shughuli za kilimo”alisema Mahembe Mayumba mkazi wa Kijiji cha Igegu
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amewataka Wataalam wa Ardhi watakaohusika na zoezi la uthamini na upimaji wa eneo litakojengwa Kiwanja hicho cha Ndege kufanya zoezi hilo kwa kufuata haki na sheria za nchi.
“Nimewaagiza wataalam watakaohusika kufanya zoezi la tathmini na kulipa fidia kwa kumuogopa Mungu, watende haki, kila ambacho mwananchi anapaswa kufidiwa wahakikishe kinafidiwa kwa mujibu wa sheria; tumekubaliana wataalam watavaa vitambulisho ili watambuliwe na ikitokea mtu akihujumu zoezi hili iwe rahisi kumfahamu na kuchukua hatua” alisema Kiswaga.
Akizungumzia suala la taarifa ya uthamini kutolewa mapema kwa wananchi, Kiswaga amesema kuwa zoezi hilo litafanyika kwa muda wa mwezi mmoja na wiki mbili na baada ya hapo wenye maeneo watapewa taarifa.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga Bi.Easter Dotto Madale amesema Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa utawasaidia wananchi kupata usafiri wa anga ambao ni wa haraka, uhakika na salama, huku akisisitiza kuwa kiwanja hicho kitakapoanza kujengwa wananchi hususani vijana watapata ajira kwenye kazi za ujenzi na wanawake watajiajiri katika kazi za kupika na kuuza vyakula
Naye Afisa Ardhi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Bi. Bi. Cecilia Mwing’uri amesema Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Nchini (TAA) imeshatoa fedha kwa ajili ya tathmini, uthamini na upimaji wa maeneo Kiwanja kitakapojengwa na mara baada ya zoezi hilo kukamilika wananchi wanaohusika watalipwa fidia.
Bi.Cecilia amewahakikishia wananchi wa Vijiji vya Igegu na Ng’arita kuwa watalipwa fedha zao zote mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki , kwa kuwa Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Nchini (TAA) imetenga fedha hizo kwa ajili ya fidia ya Kiwanja cha Ndege cha Simiyu.
Kwa mujibu wa Meneja wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga Bi.Beaster Dotto Madale Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Mkoani Simiyu kitakapokamilika kitakuwa ni miongoni mwa Viwanja vikubwa hapa nchini ambavyo vina uwezo wa kupokea ndege kubwa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-http://simiyuregion.blogspot.com/2018/09/wananchi-wilayani-bariadi-waridhia.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa