Wananchi Mkoani Simiyu wamehimizwa kwenda kushuhudia mashindano ya Baiskeli na Ngoma za Asili yatakayofanyika kesho Jumapili katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mratibu wa Mashindano hayo yanayotambulika kama Simiyu Jambo Festival ambayo yanadhaminiwa na Kampuni ya Jambo Food Products, Ndg.Kulwa Mtebe amesema washiriki wa mbio za baiskeli kutoka mikoa mbalimbali wameshawasili Mjini Bariadi na wamejiandaa vizuri kwa ajili mashindano.
Aidha, amesema Mgeni Rasmi katika tukio hilo(Simiyu Jambo Festival) la Kihistoria Mkoani Simiyu ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Tulia Ackson ameshawasili Mkoani kwa ajili ya mashindano hayo.
Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Simiyu, Edson Mwakihaba amesema Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba watumiaji wa barabara wanazingatia sheria za usalama barabarani na askari watakuwepo katika vituo vyote ambavyo washiriki wa mbio za baiskeli watapita.
Rais wa Chama cha Baiskeli Taifa Godfrey Mhagama amesema Chama hicho kupitia kamati yake ya Ufundi kitakahikisha kanuni na taratibu za mchezo wa mbio za baiskeli zinasimamiwa na kufuatwa katika mashindano hayo.
Mhagama ameongeza kuwa Wachezaji wahakikishe wanacheza katika viwango vinavyotakiwa kwa kuwa vigezo vyote vitavyozingatiwa ikiwa ni pamoja na kasi ya mchezaji na muda anaoutumia katika kukamilisha mbio kwa umbali uliopangwa, ambayo pia itakuwa ni njia ya kupata wachezaji wanaoweza kuwakilisha Taifa katika Mashindano ya Olimpiki.
Kwa upande wake Meneja Masoko wa Kampuni ya Jambo Food Products Anthony Paul amewahakikishia washiriki kuwa zawadi zote zilizopangwa kwa washindi katika makundi yote matatu (wanaume, wanawake, walemavu) ziko tayari ambayo ni pikipiki itakayotolewa kwa mshindi wa kwanza(wanaume) na fedha taslimu zaidi ya shilingi Milioni nane zitakazotolewa kwa washindi wengine.
Naye Emmanuel Mollel mshiriki wa mashindano ya mbio za Baiskeli kutoka mkoa wa Arusha amesema washiri kutoka katika mkoa huo wamejipanga kikamilifu na kiushindani kuhakikisha wanapata ushindi.
Tatu Malulu mshiriki wa mbio za Kilometa 80 kutoka katika Mkoa wa Mwanza amesema amekuwa akifanya mazoezi siku zote ambayo yamemuimarisha hivyo akathibitisha kuwa kutokana na maandalizi hayo anatarajia ushindi na ametoa wito kwa Wachezaji kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi siku zote maana ndio siri ya kufanikiwa kwao.
Zaidi ya washiriki 160 kutoka katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Geita na Arusha wanatarajia kushiriki mashindano hayo ambayo yatagawanyika katika makundi matatu; wanaume Kilometa 200, wanawake Kilometa 80 na Watu wenye Uemavu Kilometa 05.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa