Wananchi wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu wameipongeza Serikali kwa kuwajengea mahakama ya Wilaya ya Bariadi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu jambo ambalo limewapunguzia adha ya kutumia gharama na muda mrefu kwenda kufuata huduma za mahakama katika mkoa wa Shinyanga kama ilivyokuwa awali.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo la mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu na Mahakama ya Wilaya ya Bariadi ambayo ilifanyika Juni 22, 2020 Mjini Bariadi, Bw. Zengila Nyoni mkazi wa Bariadi ameomba watumishi wa mahakama kutoa huduma kwa kuzingatia misingi ya haki ili umuhimu wa uwepo wa mahakama uonekane kwa wananchi.
“Tunaishukuru Serikali kutujenge jengo zuri la mahakama, sasa hivi hatutasafiri kwenda Shinyanga kufuata huduma za mahakama ya hakimu mkazi ni hapa hapa tu; niwaombe mahakimu na majaji kutoa haki kwa wananchi ili tufurahie uwepo wa jengo hili zuri, maana haitakuwa na faida kama tumejengewa jengo zuri halafu huduma zisiwe nzuri,”alisema Nyoni.
Awali akizungumza katika uzinduzi huo Jaji kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewashauri Wakuu wa Wilaya na Mikoa nchini kutumia kamati za maadili za wilaya na mikoa ambazo wao ni wenyeviti wa kamati hizo kuwajadili mahakimu ambao wanaenda kinyume na maadili ya utumishi wa Umma.
“ Ni aibu kwa Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa kusema kuwa hamtaki hakimu fulani kwenye eneo lake wakati yeye ndiyo mwenyekiti wa kamati ya maadili ya wilaya au mkoa, mahakimu wasio waadilifu wafikisheni kwenye kamati za maadili, zile kamati zinajuimisha watu wengi wazuri; niendelee kuwasihi watumishi wa Mahakama kujiepusha na vitendo vilivyo kinyume na maadili,” alisema Jaji Feleshi.
Katika hatua nyingine Jaji Kiongozi amewaomba wakuu wa mikoa nchini kusaidia Magereza mikoani mwao kupata vifaa vya TEHAMA ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania za kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao, ambapo amebainisha kuwa tayari vifaa vya TEHAMA vimeshawekwa kwenye mikoa mbalimbali nchini na endapo wadau hao wa Mahakama wataziwezesha Magereza, kazi hiyo itafanyika kwa urahisi.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Shinyanga, Mhe. Gerson Mdemu amesema ujenzi wa jengo la mahakama ya wilaya ya Bariadi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, utasaidia kuokoa fedha iliyokuwa ikitumika kulipa pango na itatumika kutoa huduma katika maeneo mengine.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesisitiza uadilifu kwa watumishi wa mahakama, huku akibainisha kuwa kujenga kwa mahakama kutawasaidia wananchi kupata huduma karibu na kuokoa rasilimali fedha na muda waliokuwa wakitumia kufuata huduma mkoa wa Shinyanga.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mahakama ya wilaya ya Bariadi na Mhakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu, Leonald Maufi amesema ujenzi umegharimu zaidi ya shilingi milioni 800.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/06/wananchi-waipongea-serikali-kuwahjengea.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa