Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthnony Mtaka ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa mkoani hapa kwenda kujiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura, kugombea nafasi mbalimbali na hatimaye kwenda kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 ili wapate viongozi waadilifu.
Mtaka ametoa wito huo wakati akizungumza na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Petro Mwanhuzi wilayani Meatu, baada ya ibada ya misa takatifu Oktoba 06, 2019 ambapo alibainisha kuwa wananchi wanapaswa kuchagua viongozi waadilifu na wacahapakazi ambao watasimamia vizuri fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
“Kuanzia tarehe nane mwezi huu uandikishaji unaanza nendeni mkajiandikishe na wote wenye sifa chukueni fomu za kugombea nafasi mbalimbali na kujitokeza kupiga kura siku ya tarehe 24 Novemba ili mpate viongozi bora, tumekuwa tunapata migogoro mingi ya ardhi, fedha za miradi kutotumika inavyotakiwa na moja ya sababu ni vongozi wasio waadilifu, kajitokezeni mchague waadilifu, “ alisema.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa wananchi mkoani Simiyu kusomesha watoto wao na kuona umuhimu wa kuchangia ujenzi wa miundombinu ya elimu ikiwemo vyumba vya madarasa na mabweni ambayo yatawapunguzia watoto wa kike kutembea mwendo mrefu.
Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Petro Mwanhuzi wilayani Meatu, Paroko Robert Walwa amesemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kusisitiza umuhimu wa kupenda elimu jambo ambalo amesema hata Biblia Takatifu imesisitiza kuishika elimu maana ndiyo chimbuko la imani, hivyo ni vema wananchi wakazingatia elimu ili imani zao ziimarishwe.
Naye mmoja wa waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Petro Mwanhuzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Jennifer amesema wananchi wanamshukuru Mkuu wa Mkoa kwa jitihada anazozifanya katika mkoa ambazo zimekusudia kuinua mkoa kielimu na akabainisha kuwa watashirikiana na Serikali katika kuhakikisha malengo ya kuinua sekta ya Elimu yanatimia ikiwemo kuongeza ufaulu.
Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Bi. Jeniffer amesema atahakikisha anajiandikisha na kupiga kura siku ikifika ili aweze kutumia vema haki yake ya msingi ya kuchagua kiongozi anayemtaka na si wa kuchaguliwa na watu wengine.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/10/mkuu-wa-mkoa-wa-simiyu-mhe.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa