Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Angelina Mabula amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani Simiyu kuwasimamia watumishi wa Idara ya Ardhi na kuhakikisha wanapima maeneo na kutoa hati miliki kwa wananchi.
Mhe.Mabula ameyasema hayo wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu ambayo imelenga kufuatilia utekelezaji wa maelekezo mbalimbali aliyoyatoa wakati wa ziara yake Novemba 2017, mwenendo wa ukusanyaji wa kodi za ardhi na kukagua Jengo la Kanda ya Ardhi Simiyu itakayohudumia Mikoa ya Simiyu,Shinyanga na Mara,
“Mtumishi aliyeajiriwa kama surveyor (mpima ardhi) hana sababu za kukaa ofisini kuanzia saa 1:30 asubuhi mpaka saa 9:30 alasiri wakati kazi zake nyingi ziko uwandani; Mwisho atajikuta amepima viwanja 58 mwaka mzima, maana yake ni kwamba atakuwa hajajua wajibu wake, wakurugenzi badilikeni katika kuwasimamia watumishi wa sekta ya ardhi” amesema Mabula
Amesema ikiwa Watumishi wa Idara ya Ardhi wakitimiza wajibu wao Ardhi ikapimwa, wananchi wakapewa hati miliki ya maeneo yao ya viwanja na mashamba; migogoro itapungua, Serikali itakusanya maduhuli kupitia kodi ya Ardhi na uendelezaji wa miji utafanyika katika mpango mzuri
Pamoja na kupima maeneo na kutoa hati miliki, Mhe.Naibu Waziri amesema Idara ya Ardhi inapaswa kuhakikisha wananchi waliomilikishwa maeneo wanajenga kwa kuzingatia sheria Namba 8 ya mwaka 2007 ya Mipango Miji, ili kuepukana na ujenzi holela unaopelekea kuwa na miji isiyopangwa.
Aidha, Mhe.Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amesisitiza maeneo yote ya Taasisi za Serikali yapimwe na kutolewa hati miliki ili kuyalinda na uvamizi.
Sanjali na hilo, Mhe.Naibu Waziri amewataka wataalam wa Ardhi kukusanya maduhuli ya Serikali yatokanayo na kodi za ardhi kwa kutumia mifumo ya Kielektroniki iliyowekwa katika kufuatilia na kuhakikisha wananchi wote wanaostahli kulipa kodi ya ardhi wanalipa kwa wakati.
Naibu Waziri ameelekeza Kamati za Halmashauri zinazosimamia Ardhi zihakikishe zinaifanya agenda ya Makusanyo ya maduhuli kuwa ya kudumu katika vikao vyao vya kila robo, ili kila wanapokutana itolewe taarifa ya hali ya makusanyo, wananchi waliopewa notisi na wale wanaotakiwa kupelekwa katika mabaraza ya Ardhi ya Wilaya kwa kushindwa kulipa kodi ya ardhi kwa wakati.
Akiwasilisha taarifa ya Wilaya ya Bariadi Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe.Festo Kiswaga amesema Halmashauri zote mbili zinazounda Wilaya ya Bariadi zinaendelea na kuhamasisha wananchi kupima maeneo yao na kupata hati miliki ili kuongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia kodi ya Ardhi, ambapo Halmashauri ya Wilaya Bariadi pekee kwa mwaka 2017/2018 inatarajia kupima viwanja 2400 katika Vituo vya Kibiashara vya Nkololo,Dutwa na Ngulyati.
Naye Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Kanda, Makwasa Biswalo amesema Mtalaam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amefika Mkoani Simiyu kwa ajili ya kutoa mafunzo ya mfumo wa ukusanyaji wa kodi za Ardhi, kwa watumishi wa Halmashauri zote ambao utawawezesha kutengeneza ankara (bill) ya makusanyo ya kodi na tozo zote.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ameshukuru Wizara ya Ardhi kwa kuona Umuhimu wa kuanzisha Kanda ya Ardhi ya Simiyu na akaomba Wizara ifanye utaratibu wa kumleta Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Maswa kutokana na aliyekuwepo kasimamishwa kazi, hali iliyopelekea mashauri mengi kutofanyiwa kazi.
Msajili Msaidizi wa Baraza la Ardhi Kanda ya Ziwa, Dorothy Moses amesema kuanzia mwezi Septemba 2017 atakuwepo Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Maswa ambaye atasikiliza kesi, ambapo pia ameleeza kuwa Wizara ina mpango wa kuanzisha mabaraza mawili ya Ardhi na Nyumba katika Wilaya ya Bariadi na Busega ambayo yataanzishwa muda wowote baada ya kupatikana majengo kwa ajili ya Ofisi.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Angelina Mabula(Mb) yuko katika ziara ya siku mbili Mkoani Simiyu ambapo akiwa Mjini Bariadi amefanya kikao na Viongozi, wataalam wa Ardhi na Watendaji wa Kata,Mitaa na Vijiji wa Halmashauri ya Mji Bariadi na Halmashauri ya Wilaya Bariadi kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya watumishi wa Idara ya Ardhi Mkoa na Wilaya na Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji wa Wilaya ya Bariadi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Mhe.Angelina Mabula(Mb) (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akiwaasilisha taarifa ya Wilaya hiyo kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Mhe.Angelina Mabula(Mb)(wa tatu kushoto)wakati akiwa katika Ziara ya siku Mbili Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akiwaasilisha taarifa ya Wilaya hiyo kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Mhe.Angelina Mabula(Mb)(wa tatu kushoto)wakati akiwa katika Ziara ya siku Mbili Mkoani Simiyu.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Bariadi(kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Mhe.Angelina Mabula(Mb)(kulia) kuhusu jengo lililoandaliwa kwa ajili ya Ofisi ya Ardhi Kanda ya Simiyu ambayo inatarajia kuanza kazi hivi karibuni, ambayo itahudumia mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga.
Mkurugenzi wa mji wa Bariadi, Ndg.Melkizedek Humbe akitoa maelekezo kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Mhe.Angelina Mabula(Mb) wakati alipotembelea Ofisi ya Idara ya Ardhi ya Halmashauri hiyo kujionea namna inavyokusanya mapato yatokanayo na Ardhi, wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa