Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019, Ndg. Mzee Mkongea Ali ametoa wito kwa viongozi wilayani Meatu kuwasaidia wakulima wa pamba kupata zana bora za kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji na wilaya hiyo iendelee kuwa kinara katika uzalishaji wa zao la pamba nchini.
Ndg. Ali ameyasema hayo wakati Mwenge wa Uhuru ulipopita na kukagua Shamba la Mbegu bora ya pamba lenye ukubwa wa ekari 13 katika Kijiji cha Mwabusalu ambapo alimpongeza mkulima Jidayi Charles na kumtunuku cheti cha kumtambua kama mkulima bora.
“Ninampongeza sana Bwana Jidayi maana ni wazee wachache sana wanaojihusisha na kilimo ni vizuri mkachukua jitihada za makusudi kumsaidia apate zana za kisasa, kama analima ekari 13 akiwa hana trekta nina uhakika akiwezeshwa atafanya vizuri zaidi, kama mmeshaanza utaratibu wa kumpatia mkopo uharakishwe ili kiwango cha uzalishaji kiweze kuongeza zaidi” alisema Mzee Mkongea Ali.
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani amesema wilaya ya Meatu ndiyo wilaya kinara katika uzalishaji wa pamba nchini ambapo amebainisha kuwa katika msimu wa mwaka 2018/2019 ilizalisha takribani kilo milioni 31 za pamba na akaeleza kuwa mkakati wa wilaya ni kuendelea kuwasaidia wakulima kwa utaalam na mikopo za kununua zana bora ili waweze kuzalisha kwa tija zaidi.
Akitoa taarifa ya mradi wa shamba hilo, Afisa Kilimo wa Wilaya ya Meatu, Bw.Thomas Shilabu amesema uzalishaji wa zao la pamba unakabiliwa na changamoto ya baadhi ya wakulima kulima wa kilimo cha mazoea kwa kusia mbegu na kupalilia maotea.
Kwa upande wake Bw. Jidayi Charles amesema kwa sasa anatumia trekta ya kukodi kulima shamba lake lenye ukubwa wa ekari 13 ambalo linachangia kuchelewesha uandaaji wa shamba kwa kuwa linatumiwa na wakulima wengi, lakini endapo atakapata trekta lake litamrahisishia kuandaa shamba mapema na kwa urahisi zaidi.
Pamoja na kutembelea mradi wa shamba za kuzalisha mbegu bora za pamba, Mwenge wa Uhuru ukiwa Wilayani Meatu umezindua vyumba viwili vya maabara shule ya Sekondari Mwandoya, kutembelea mradi wa maji wa SangaItiinje na kupanda miti katika Chanzo cha maji, kukagua klabu ya wanafunzi ya wapinga RUSHWA na Klabu ya wanafunzi ya kupambana na mimba za utotoni shule ya msingi Isengwa.
Wakati mwenge wa uhuru ulipopita kuona shughuli za klabu ya mapambano dhidi ya mimba za utotoni, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ameupongeza uongozi wa wilaya ya Meatu kuanzisha klabu hizo shuleni na akatoa wito kwa wataalam wa Ustawi wa Jamii na Dawati la jinsia na vyombo vya dola kutowahurumia wote wanaobanika kusababisha mimba za utotoni.
Aidha, ulifungua Nyumba ya kulala wageni TS Lodge, kukagua shughuli za kikundi cha vijana wajasiriamali, kukagua shughuli za mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya mimba za utotoni na mapambano dhidi ya malaria.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU MBIO ZA MWENGE WA UHURU MEATU FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/05/wakulima-wakiwezeshwa-zana-bora-za.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa