Bodi ya Mkonge Tanzania imekutana na uongozi wa mkoa wa Simiyu na baadhi ya watendaji na wataalam wa kilimo kwa lengo la kujadili mwongozo wa kilimo cha mkonge mkoani hapa lengo likiwa ni kuhakikisha mkulima anazalisha mkonge bora na wenye thamani katika soko.
Akikabidhi mwongozo huo kwa katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga na baadaye akawakabidhi maafisa Kilimo, Mratibu mkuu wa utafiti na masoko, Bw Hassan Kibarua amesema ni vema wataalam wa kilimo wakatoa elimu kwa wakulima wa mkonge juu ya kuzingatia ubora kuanzia uzalishaji ili usipungue thamani.
"Mkonge unatakiwa kuchakatwa si zaidi ya masaa 48 tangu kukatwa lakini kuna wakati mkulima anachakata mkonge uliokatwa zaidi ya siku tano, unakuwa umepungua ubora na unapofika sokoni unakuwa haupo kwenye daraja la ubora wa 3L ambalo lina bei ya juu, " alisema Kibarua.
KIbarua ameongeza kuwa pia wakulima inabidi waelekezwe namna ya kuchakata na kusafisha mkonge ili wasipeleke sokoni mkonge wenye uchafu (maganda) kwani makosa kidogo yanapelekea kushuka kwa thamani ya zao hilo.
Ameongeza kuwa mkonge unasoko la uhakika ndani na nje ya nchi kutokana na kuongezeka kwa matumizi kutoka kwenye yale ya awali ya kutengeneza kamba na magunia; sehemu ya matumizi mengine ni kutengeneza mapambo ya nyumba, mabaki yake kutengeneza gesi na chakula cha mifugo
Akizungumzia umuhimu wa kupima afya ya udongo ili kuongeza uzalishaji wa mkonge, mratibu wa utafiti wa udongoTanzania kutoka TARI- Mlingano Dkt. Sibaway Mwango, amesema ni vema maafisa ugani wakatimiza wajibu wao na wawaunganishe watafiti na wakulima ili wakulima waweze kulima kwa tija.
"Kila mmea una aina fulani ya udongo ambao unahitaji na kiasi fulani cha tindikali kisichozidi , hivyo ni muhimu wakulima kupima afya ya udongo kabla ya kupanda mazao ili kujua aina ya virubishi vilivyopo na aina ya mbolea inayotumika Afya ya udongo ni muhimu zaidi kwa kilimo chenye tija," alisema Dr Mwango.
Aidha amesema, afya ya udongo ni lazima ilindwe kwa kupanda mazao ya mikunde katika mashamba ya mkonge, kuepuka matumizi ya mbolea yasiyo sahihi yanayo sababisha kuharibu udongo, ambapo alibainisha kuwa hali hiyo inachangia wakulima kutopata mavuno mengi na yenye ubora uliokusudiwa .
Katika mkoa wa Simiyu zao la mkonge tayari limeanza kulimwa katika baadhi ya maeneo hasa katika wilaya ya Meatu na Maswa ambapo wakulima wanaojishughulisha na kilimo hicho wametoa wito kwa wakulima wenzao kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa zao hilo linalimwa wakati wowote na linastahimili katika hali zote.
"Kilimo cha mkonge hakimtupi mtu maana mkonge haubagui ukame wala mvua nyingi kwa hali yoyote ni lazima uvune na kizuri zaidi ninachanganya na mazao mengine yaliyoko kweye msimu na sijaona shida yoyote,” alisema Bw. Mabula Mipawa
"Ukiangalia uchumi wangu wa sasa na hapo awali kuna mabadiliko sana sasa ninalima kilimo ambacho kinaniingizia pesa muda wowote hadi nimefikia hatua ya kuweza kupeleka watoto wangu shule na kuwa na uchumi mzuri,"alisema Mizwazwa Kidia mkulima wa mkonge kata ya Mwasengela.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI TAFADHALI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/09/wadau-wa-kilimo-simiyu-wajadili.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa