Wadau wa Elimu mkoani Simiyu wamekiri kuwa kambi za kitaaluma zimekuwa na mchango mkubwa katika kuuwezesha mkoani huo kushika nafasi ya kumi Kitaifa katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2018, kutoka nafasi ya 26 mwaka 2017.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha tathmini ya Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2018 kilichofanyika Julai 24, Mjini Bariadi ambapo pia walimu wa Kidato cha Sita waliowezesha wanafunzi kufaulu kwa alama A na B katika masomo yao wamepongezwa na kupewa zawadi ya fedha taslimu na vyeti.
Kikao hiki kimewashirikisha viongozi na Watendaji wa Serikali ngazi ya Mkoa na Wilaya, Wakuu wa Shule na walimu wa shule za Sekondari za kidato cha tano na sita, wadhibiti ubora, Maafisa Elimu Wilaya na Kata, Wenyeviti wa Bodi za Shule, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Chama cha Walimu na wadau wengine.
Baadhi ya wadau waliochangia katika tathimini hiyo wamempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa kuanzisha wazo la kuwa kambi za kitaaluma ambazo zimeleta mafanikio makubwa na kutoa maoni ya namna ya kuboresha na kuzifanya kambi hizi kuwa mkakati endelevu katika kuinua ubora wa elimu mkoani Simiyu.
“Nampongeza sana mkuu wetu wa Mkoa kuja na wazo hili la kuwa na kambi za Kitaaluma na Mkuu wa Mkoa amesema ni agenda ya kudumu katika mkoa , kama walimu, wazazi, wanafunzi, sisi viongozi na wadau wengine wa elimu katika Mkoa wetu tukiendelea kushirikiana, kambi hizi zitabadilisha mfumo wa elimu na kuufanya mkoa ung’are katika sekta ya elimu” Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe.
“Kambi za Kitaaluma zimechangia kuufikisha mkoa kwenye nafasi ya 10 Kitaifa lakini nashauri iundwe kamati ya ndogo ya Maafisa Taaluma kutathmini mazuri na changamoto za kambi za kitaaluma ili tuweze kuboresha zaidi na kuufanya mkoa kufanya vizuri zaidi” Mwl.Baraka Owawa Katibu Chama cha Walimu Wilaya ya Bariadi.
Nao viongozi wa madhehebu ya dini walioshiriki katika kikao hicho cha tathmini wamesema wanaunga mkono juhudi za Serikali katika maendeleo ya elimu na wakaahidi kushirikiana na Serikali kwa kuwa hata vitabu vya dini navyo vinahimiza kupenda na kuthamini Elimu.
Afisa Taaluma wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Onesmo Simime akitoa tathmini ya matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2018 amesema idadi ya wanafunzi waliopata daraja la I imeongezeka kutoka wanafunzi 43 mwaka 2017 na kufikia 119, daraja la II imeongezeka kutoka 304 mwaka 2017 hadi 451, daraja III toka 325 mwaka 2017 hadi 381.
Aidha, amesema idadi ya wanafunzi waliopata daraja sifuri imepungua kutoka kutoka wanafunzi 29 mwaka 2017 hadi wanafunzi 14 mwaka 2018 ambapo amebainisha kuwa shule sita kati ya 11 mkoani humo zimefanikiwa kuondoa daraja sifuri mwaka 2018.
Amesema pamoja na kambi za Kitaaluma mkoa uliweka mikakati ambayo pia imechangia kuongeza ufaulu kuutoa kwenye nafasi ya 26 mwaka 2017 hadi 10 Kitaifa mwaka 2018, ambayo ni kuhakikisha walimu wanafundisha vipindi vyote na kufidia vilivyopotea na kufanya mtihani wa utimilifu (Mock) wa Mkoa na kanda uliowasaidia walimu kubaini mada zenye changamoto na kufanya mapitiao ya mada hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amewapongeza walimu,wazazi wanafunzi na wadau wote wa elimu waliofanikisha mkoa kufanya vizuri katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2018, huku akisisitiza kuendelea kuweka mikakati ya kuboresha uendeshaji wa kambi za kitaaluma ili waweze kufikia lengo walilojiwekea la kufikia ‘single digit’ nafasi ya 1-9.
Katika kikao hicho pia Mtaka ameagiza kuwa muda wa wanafunzi wa madarasa ya mtihani katika Shule za Sekondari za Serikali(Kidato cha nne na cha sita)kuzimiwa taa utakuwa saa sita usiku siyo saa nne usiku, hivyo akiwataka walimu kuweka utaratibu wa viongozi wa wanafunzi kuendelea na ratiba kwa niaba yao baada ya ratiba ya walimu inayoishia saa nne usiku.
Wanafunzi wa kidato cha sita mwaka 2018 walikaa katika kambi za Kitaaluma kwa muda wa siku 10 mwezi Aprili, aidha wanafunzi wa Kidato cha nne na Darsa la saba wa mwaka 2018 waliwekwa katika kambi za kitaaluma mwezi Juni kwa siku 21 kwa ajili ya kujiandaa na mitihani yao ya Taifa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI ZA TUKIO HILI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/07/wadau-wa-elimu-wakiri-kambi-za.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa