Mhe.Kafulila ameyasema hayo leo, wakati alipotembela mgodi wa EMJ, Dutwa wilayani Bariadi. Mhe kafulila amefanya ziara hiyo ili kukutana na kutatua kero za wachimbaji. Wakizungumzia kero zao, Wachimbaji hao wametaja kero hizo kuwa ni pamoja na kukatazwa kuchimba kwenye baadhi ya maeneo, uwepo wa mwekezaji mchina ambaye ameanza kujenga uzio na hivyo kuhofia uhuru wao wa kuchimba madini kwenye eneo hilo na Maduara yaliyotelekezwa kurudishwa kwa mwenye leseni, huku wao wakitafuta nguvu zaidi za kuendelea na uchimbaji.
Akijibu hoja hizo Mhe. Kafulila alimtaka Mwakilishi toka ofisi ya Madini bwana Lucas Mwakulo, kujibu kero hizo na kueleza sheria inasemaje kuhusu maduara yaliyotelekezwa. Bw.Mwaluko alieleza kuwa ni kweli kwamba kuna eneo ambalo ofisi ya Madini imekataza uchimbaji wa madini na hiyo ni kwa sababu za kiusalama. Suala la kiusalama lipo juu ya kila kitu. Hairuhusiwi mchimbaji yeyote kuchimba katika eneo ambalo ni hatarishi.Aidha Serikali imetoa maelekezo kuwa mchimbaji anaweza kupewa kibali cha siku 30 ili apumzike na kukusanya nguvu, siku hizo zikipita shimo linarudishwa kwa mwenye leseni.
Nae katibu wa wachimbaji Bw. Ramadhani Faida, alieleza kuwa ni kweli kwamba kuna duara 5 zilizosimamishwa uchimbaji na duara hizo ni 286A, 203A,190,101B na duara namba 237B. Akizungumzia sababu ya kufungwa mashimo hayo mkaguzi Mkuu (chief Inspector) Bw. Charles Lyaganga alizitaja sababu hizo kuwa ni Changamoto ya maji na ajali za gesi.“Sisi ndio tunatoa mapendekezo ofisi ya Madini kuwa shimo gani lifungwe baada ya ukaguzi. Tarehe 16/01/2022 tulitangaza maduara 11 kuwa hatarishi”. Amesema Lyaganga.
Mhe. Kafulila ameitaka ofisi ya madini kwa kushirikiana na Mkaguzi ,kubainisha Maduara yaliyotekelezwa kama yapo, na endapo yapo basi mabango yakawekwe kwenye maduara hayo mara moja na baada ya siku 30 yarejeshwe kwa mwenye leseni. “Yale maeneo ambayo ni hatarishi,kimsingi kwenye hayo maeneo uchimbaji usiendelee, usimamishwe,kwani uhai wenu ni muhimu kuliko madini.Hayo maeneo msiende kama mnaenda basi muende kwa kibali cha afisa madini.Mpate ridhaa ya afisa madini”. Ameagiza Mhe. Kafulila.
Aidha Mhe. Kafulila ametoa ruhusa kwa wachimbaji kuendelea na uchimbaji madini kwenye maeneo yaliyo salama ili mradi wazingatie, kanuni, sheria na taratibu.Mkuu wa Mkoa amemwelekeza inspekta Lyaganga kufanya kazi kwa umakini na kwa ukaribu na ofisi ya madini. “Wachimbaji fuateni taratibu, sio mnaacha maduara yenu bila kufuata taratibu halafu baadae mnavizia fidia. Kwa maeneo ambayo yapo nje ya maeneo hatarishi endeleeni na uchimbaji ”.Amesema Kafulila.
Akizungumzia suala la uwepo wa Wachina, Mhe. Kafulila alieleza kuwa uwepo wa Wachina hao ni makubaliano kati ya mwenye leseni na Wachina, ili waweze kufanya utafiti na kuona ni kwa jinsi gani na kwa kutumia teknologia ya juu wanaweza kupata madini zaidi, kwani wachina hao ni wazoefu na wamefanya kazi katika migodi mingine kama vile Geita.
Aidha ujenzi wa uzio kwenye eneo hilo ni kwa sababu za kiusalama, kama ilivyoelezwa na mwakilishi kutoka ofisi ya madini ambaye alieleza kuwa maelekezo yalishatolewa kuwa kwenye kila mgodi ni lazima kuwe na uzio ili kuepuka uvamizi na wizi mgodini (Manyani). Mhe.Kafulila alisisitiza kuwa, pamoja na uwepo wa uzio huo wachimbaji, wataruhusiwa kuendelea na uchimbaji madini.Mwisho.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa