Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana UVCCM Taifa Kheri James amewaasa viongozi wa dini ,chama na Serikali kutotofautiana lugha kuhusu haki za wananchi katika kukomesha dhuluma na pia wawakemee wanaokwamisha juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.
James amesema hayo katika futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka katika viwanja vya ofisi ya mkoa, na kuhudhuriwa na waumini wa Dini ya Kiislamu wakiongozwa na Shekh Mahamudu Kalokola ,viongozi wa madhehebu mbalimbali na viongozi wa chama na serikali ,ikiwa ni desturi yake kila mwaka kujumuika pamoja katika kipindi cha mfungo mtukufu wa Ramadhan.
“Maendeleo yanayofanywa sasa ni kwa ajili ya watu wote sisi kama viongozi tunao wajibu wa kushiriki ili tuweze kuhakikisha kuwa yanafikiwa kwa wakati, viongozi wa dini, chama na Serikali tusitofautiane lugha katika kutetea haki za wananchi, tuhakikishe tunasimamia wananchi wetu wanapata haki na dhuluma inakomeshwa” alisema James.
James amesema viongozi wa madhehebu ya dini wana mchango mkubwa kwa Serikali katika kuhimiza maendeleo kupitia makanisa na misikiti ,hivyo ni vema kuendelea kuliombea taifa kudumisha amani pasipo kutofautiana na chama na Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amewashukuru viongozi wa dini kwa namna wanavyoshirikiana na Serikali katika masuala mbalimbali , huku akiwaomba kuendelea kusaidia katika malezi ya watoto hasa katika mkakati wa mkoa wa kuinua kiwango cha ufaulu madarasa la mitihani, ambapo Kidato cha nne na darasa la saba wapo katika kambi za Kitaaluma.
“Watoto wetu wa kidato cha nne na darasa la saba wako katika kambi za kitaaluma kwa ajili ya kujiandaa na mitihani ya Taifa, sisi kama Serikali tumetoa nafasi ya kama nusu saa kwa watoto kushiriki ibada kila siku katika kambi hizo, tunaomba viongozi wetu wa dini mfike kwa ajili ya kuwausia na kuwasisitiza kusoma kwa kuwa tunahitaji watoto wetu wafanye vizuri “ alisema.
Shekhe wa Mkoa wa Simiyu Mahamudu Kalokola ameishukuru Viongozi wa Serikali Mkoani humo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Anthony Mtaka kwa namna wanavyoshirikiana na Madhehebu yote ya dini naye akaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika Nyanja mbalimbali za maendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Deo Ndejembi ambaye yupo SIMIYU na viongozi wa vikundi vya vijana Kongwa kwa lengo la kujifunza Simiyu ilivyofanikiwa kwa miradi ya vijana, akiwa katika futari hiyo amesema Simiyu imejipambanua vema katika masuala ya vijana hususani katika uzalishaji mdogo mdogo jambo ambalo liwawafanya waje kujifunza ili waweze kuwasaidia vijana wa Kongwa kuanzisha miradi endelevu na yenye tija.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KATIKA TUKIO HILI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/06/viongozi-mkoani-simiyu-waaswa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa