Viongozi na Watendaji Watakiwa kutowabugudhi Wafanyabishara
Serikali imewataka viongozi wa kisiasa pamoja na watendaji wa Serikali kutotumia vibaya madaraka yao kwa kuwanyanyasa na kuwasumbua wafanyabishara hasa wazawa waliowekeza ndani ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda akiwa mkoani Simiyu, wakati wa Mkutano wa Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa pamoja na Tovuti ya Mkoa.
Profesa Mkenda amesema viongozi hao wanatakiwa kuwajengea wafanyabiashara mazingira rafiki yatakayowawezesha kufanya biashara zao kwa amani ili kuweza kukuza uchumi wa Taifa na kuongeza ajira kwa vijana.Aidha, amewasihi viongozi wote wa Serikali ngazi za Mikoa na wilaya hapa nchini kujivunia uwepo wa wajasiriamali na wafanyabiashara wakubwa ambao ni wazawa kwani wao ni chachu ya kuongezeka kwa ajira za vijana.
Amesema kuwa si vyema wafanyabishara kutukanwa, kutolewa lugha zisizokuwa sahihi na kuonekana kama wana uadui na Serikali, badala yake watengenezewe mazingira mazuri ili waweze kulipa kodi na kufuata sheria na taratibu za nchi.
“ Hawa wafanyabishara hasa wazawa na wajasiliamali tuwaone kama wenzetu, ndugu zetu na watu muhimu, kwani wameajiri vijana wetu, wanalipa kodi ili nchi ipate maendeleo, lakini wanatekeleza kauli mbiu ya Rais , Tanzania kuwa nchi ya viwanda, tuwathamni” alisema Adolf.
Mbali na hilo Katibu Mkuu huyo amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga maeneo kwa ajili ya wawekezaji wakubwa na wadogo kwa ajili ya kujenga viwanda.Awali akiongea katika Mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa ili Tanzania iweze kufanikiwa katika azma yake ya kuwa na viwanda lazima Serikali iwekeze kwanza katika utafiti wa fursa zilizopo.Mtaka amesema kuwa kuwekeza katika utafiti kutasaidia kutoa uthubutu wa kufanya na kutenda mambo mbalimbali yatakayoifanya nchi kuwa na uchumi wa kati na kuwaletea wananchi maendeleo.
“ Nchi hii tusingelihitaji kuona wakuu wa mikoa kuwa wabobezi katika kila sekta na badala yake wawaache wataalam na watafiti wafanye kazi zao kitaalamu ili kuepuka mvurugano wa shughuli za kimaendeleo ndani ya nchi” amesema Mtaka.Kwa upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala Kiuchumi na Kijamii (ESRF) Dk Gratian Bamwenda, amesema kukamilika kwa utafiti huo ambao umetoa mwongozo wa uwekezaji mkoani Simiyu kutatoa fursa kwa wananchi na wafanyabishara kutambua fursa na kuwekeza.
Mwongozo wa Uwekezaji Mkoani Simiyu ambao umezinduliwa rasmi leo ni matokeo ya Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala Kiuchumi na Kijamii (ESRF) katika halmashauri zote sita za mkoa wa Simiyu chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP); umebainisha takribani fursa 26 za uwekezaji katika sekta zote muhimu mkoani humo.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa