Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga amewataka wataalam kufanya ukaguzi wa matumizi ya chumvi isiyo na madini joto katika maeneo tofauti mkoani Simiyu ili kuweza kupata uhalisia wa hali ya matumizi ya chumvi hiyo na matokeo yake yaweze kuwasaidia wataalam kutoa elimu juu ya madhara ya matumizi ya chumvi kwa afya ya watumiaji.
Mmbaga ametoa agizo hilo jana Machi 03, 2021 wakati akizungumza na baadhi ya viongozi na wataalam katika kikao cha Kamati ya lishe ya mkoa kilichofanyika Mjini Bariadi kwa lengo la kujadili utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe.
“Wataalam wetu wa afya tengenezeni vigezo vya kisayansi vya ukaguzi wa chumvi isiyo na madini joto utakaotupa picha halisi ya mkoa wetu ili taarifa yetu ya ukaguzi ikitoka sisi wenyewe au mtu yeyote tukimweleza aweze kuelewa; siyo tufanye ukaguzi ili ionekane tumefanya kwa kuwa sisi kama viongozi na watalaam tuna hatari kwenye jamii yetu kwamba kuna watu watapoteza maisha na pia tutakuwa na watu ambao hawana uelewa kwa sababu tu ya kutumia chumvi isiyokuwa na madini joto,” alisema
Aidha, Mmbaga ametoa wito kwa wataalam kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa chumvi isiyo na madini joto na kuwashauri badala ya kuimwaga au kuharibu chumvi inayokamatwa baada ya kubainika kuwa inauzwa au kupelekwa kwa watumiaji pasipo kukidhi vigezo vya kiafya.
Afisa Lishe wa mkoa wa Simiyu, Dkt. Chacha Magige amesema madhara ya chumvi isiyo na madini joto ni pamoja na wajawazito kujifungua watoto ambao hawajatimiza miezi tisa, watoto kuwa na uwezo mdogo wa kiakili(kufikiri) kwa kuwa chumvi yenye madini joto husaidia katika ukuaji wa ubongo wa watoto wakiwa tumboni, kuharibika kwa mimba na kusababisha goita.
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2021/03/ukaguzi-wa-chumvi-isiyo-na-madini-joto.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa