Tuzo ya Serengeti Hifadhi Bora zaidi Afrika imetambulishwa rasmi kwa wananchi wa mikoa ya Simiyu na Mara kutoka katika maeneo yanayoizunguka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Akiitambulisha tuzo hiyo Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla Juni 18, 2019 katika Kijiji cha Robanda wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, amesema tuzo hii iwe chachu kwa wahifadhi, viongozi na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi hapa nchini.
“Tuzo tuliyoipata ya Serengeti Hifadhi Bora zaidi Afrika iwe chachu ya kutufanya tuendelee kuitangaza zaidi Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ili tuweze kushinda tuzo ya Kimataifa; Tuzo hii iwe chachu kwetu wahifadhi, viongozi na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi hapa nchini” alisema Kigwangalla.
Ameongeza kuwa Sekta ya uhifadhi ina faida kubwa zaidi ya utalii ambazo ni pamoja na kutoa hewa ya oksjeni kutoka kwenye misitu, kukamilisha mzunguko wa mvua, kutoa mahali pa wanyamapori kuishi na kusaidia zoezi la uchavushaji kwa mimea unaopelekea kuwepo chakula, hivyo shughuli za uhifadhi ziimarishwe zaidi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA kwa kazi kubwa ya uhifadhi wanayoifanya jambo ambalo limeifanya Mamlaka hiyo kutoa msaada kwa jamii, ambapo alibainisha kuwa TANAPA imechangia jumla ya shilingi milioni 100 katika ujenzi wa shule ya sekondari Simiyu maalum kwa ajili ya michezo.
Aidha, Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu ni wadau wakubwa wa uhifadhi na unaunga mkono juhuda zote za uhifadhi zinazofanywa na wizara na wadau mbalimbali wa uhifadhi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima amepongeza Kamati za Ulinzi na Usalama ya Mikoa ya Simiyu na Mara kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhakikisha kuwa zinapambana na uharibifu wowote katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hali iliyochangia hifadhi hii kuonekana bora zaidi katika Bara la Afrika.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga ambaye pia ni mhifadhi amesema tuzo hiyo I matunda ya juhudi za Serikali na wananchi katika kukomesha ujangili na uwindaji haramu na kupitia tuzo hii itachochea watalii wengi kuingia nchini.
Naye Shawezi Silas mkazi wa Kata ya Ikoma wilaya ya Serengeti amesema tuzo hiyo wananchi wameipokea kwa furaha kubwa sana na imewasaidia kuilewa maana ya uhifadhi na umuhimu wa kuzilinda rasilimali za Taifa ikiwemo wanyamapori.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/06/tuzo-ya-serengeti-hifadhi-bora-afrika.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa