Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema zoezi la kugawa pikipiki kwa maafisa ugani linafanyika ili kurudisha hadhi ya kada hiyo na kutofanya hivyo itapelekea kutofikia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa maafisa ugani wa mkoa wa Simiyu lililofanyika katika uwanja wa Halmashauri ya Mji Bariadi hivi karibuni.
"Afisa ugani ana jukumu la kupeleka matokeo ya utafiti kwa wakulima na kufundisha matumizi ya mbegu bora aidha Maafisa ugani wanajukumu la kuwafundisha wakulima mabadiliko ya hali ya hewa ili waweze kulima mazao yanayokabiliana na ukame hivyo hatuwezi kupuuza huduma za ugani tukabaki salama na tutaendelea kuwapatia vitendea kazi ili kurejesha kilimo cha kisasa,"amesema Prof. Mkenda
Aidha ameendelea kwa kuahidi kuboresha kada hiyo ili waweze kufufua mashamba darasa kwa kuwapatia mafunzo rejea na kuwanunulia simu janja Maafisa Ugani wa mikoa mitatu inayolima mazao ya kimkakati kwa ajili ya kujaza taarifa za wakulima wanapowatembelea ili kutatua changamoto zao.
"Aidha aliwataka Maafisa ugani kutunza pikipiki vizuri ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha wakulima kuzingatia kung'oa mabaki ili kumaliza magonjwa ya pamba na ambaye hajang'oa masalia atachukuliwa hatua za kisheria,"amesisitiza Prof. Mkenda
Akizungumza awali Mkurugenzi mkuu Bodi ya Pamba, Bw.Marco Mtunga ametoa shukrani kwa Waziri wa kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda kwa kukubali kuhudhuria zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa sababu ni vigumu kwa afisa ugani mmoja asiye na usafiri kutembelea kata nzima hivyo kwa kuwapatia pikipiki itasaidia kusimamia vizuri wakulima wa pamba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Mbegu za Kilimo, Tanzania Dkt. Sophia Kashenge, ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kutoa kipaumbele kikubwa kwa kazi ambazo zilikuwa hazipewi kipaumbele,ameeleza kuwa kazi ya Wakala wa Mbegu za Kilimo ni kuhakikisha mbegu zinazogunduliwa na mtafiti zinamfikia mkulima na kuzizalisha kwa wingi ili zifike kwa mkulima kuendana na uhitaji.
"Mkoa wa Simiyu umepokea mbegu za alizeti tani 114 ambapo tani 60 zimepelekwa Halmashauri ya Wilaya ya itilima, tani 34 Meatu na tani 20 Maswa kwa ajili ya kilimo cha alizeti vilevile napenda kuwafahamisha kuwa Wakala wa mbegu za kilimo wameanzisha duka la mbegu mkoa wa Simiyu,"amesema Dkt. Sophia .
Katibu mkuu wizara ya kilimo Bw. Andrea Masawe amesema ugawaji wa Pikipiki ni hatua ya utekelezaji wa kile Serikali ilichoahidi ikiwa ni kipaumbele cha tatu cha mkakati wa kuongeza tija ya kilimo nchini na ana imani kubwa kuwa uwekezaji uliofanyika una kwenda kuboresha huduma za ugani ili mkulima apate elimu ya uhakika ya kanuni bora za kilimo.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila alieleza kuwa, Mkoa wa Simiyu ni mkoa wa kilimo kwani asilimia 92 ya mkoa ni vijiji na wakazi wake ni Wakulima na katika msimu uliopita Mkoa wa Simiyu ulizalisha 61% ya Pamba yote nchini na kutoa shukrani kwa Bodi ya Pamba na Waziri wa Kilimo kwa kugawa pikipiki 86 kwa maafisa ugani.
"Niwahakikishie kuwa Afisa Ugani yeyote atakayetumia Pikipiki kufanya bodaboda Mkoani Simiyu hatakuwa mtumishi wa Serikali na Mkoa utahakikisha watumishi ambao sio waadiilifu katika vyama vya Ushirika,Ushirika unawaondoa kwa kuwa lengo la kuchukua hatua kali ni kilio cha muda mrefu cha wakulima kudhurumiwa haki zao kwa sababu utaratibu unakiukwa huku sheria ikimbana mkulima auze katika ushirika"amesema Mhe.Kafulila.
Aidha aliiomba Wizara kutoa mafunzo kwa Amcos zaidi ya 300 ili kuondoa mapungufu yaliyopo ambapo watumishi wanaonekana sio waadilifu kwa sababu ya kukosa maarifa hivyo Wizara iendelee kuwezesha mikakati ya kuinua kilimo cha Pamba ambapo kwa sasa halmashauri zinabeba mzigo wa kuwezesha mikakati hiyo.
Uzinduzi wa kitaifa wa ugawaji pikipiki kwa maafisa ugani katika mikoa inayozalisha mazao ya kimkakati, umefanyika mkoani Simiyu,katika viwanja vya Halmashauri ya Bariadi Mji ambapo jumla pikipiki 86 zilikabidhiwa kwa Maafisa Ugani.
|
|
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa