Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kuanzisha vituo vya Elimu na huduma kwa walipakodi hivi karibuni, ambavyo vitawasaidia walipakodi kupata ushauri wa masuala ya kodi pamoja na kujua haki na wajibu wao.
Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Charles Kichere Mjini Bariadi, wakati akizungumza na wafanyabiashara, Viongozi na watendaji wa Wilaya na Mkoa Mkoani Simiyu, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Elimu na Usajili kwa Walipakodi mkoani humo.
Kamishna Kichere amesema uamuzi wa TRA wa kuanzisha vituo hivyo umelenga kusogeza huduma karibu kwa walipakodi ambapo wafanyabiashara(walipakodi) watapata huduma za ushauri kuhusu masuala ya kodi bila malipo katika vituo hivyo vitakavyokuwa nje ya Ofisi za TRA.
“Tunajua elimu ni muhimu sana kwa walipakodi wetu, tunataka itolewe kwa walipa kodi kila siku siyo kwa misimu; ili kusogeza huduma karibu hivi karibuni tutaanzisha vituo vya Elimu na Huduma kwa walipakodi nje ya TRA, ambavyo vitatoa huduma ya ushauri kwa walipakodi bure” alisema Kichere
Aidha, Kichere ametoa wito kwa Wafanyabishara wa Mkoa wa Simiyu ambao ameutaja kama mkoa wenye fursa nyingi za kibiashara kujitokeza kwa wingi kujisajili katika vituo vya elimu na usajili wa walipakodi, kupitia zoezi linaloendelea mkoani humo ambalo limezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka, Mei 08, 2018.
Ameongeza kuwa ni vema wafanyabiashara wakatambua umuhimu wa kulipa kodi stahiki kwa wakati stahiki, ili Serikali iendelee kutoa huduma bora kwa wananchi kupitia kodi hizo na akasisitiza wafanyabiashara ambao bado hawajarasimisha biashara zao wajisajili na kuanza kulipa kodi .
Wafanyabishara wa Mkoa wa Simiyu wameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Simiyu kwa kufanya nao kazi kwa ushirikiano na wakaomba changamoto mbalimbali zilizopo kufanyiwa kazi ili waweze kutimiza wajibu wao kikamilifu kama walipakodi.
“ Tunaomba Ofisi ya Mkoa ya TRA iboreshwe iendane na hadhi ya Mkoa, Wilaya zetu mpya za Busega na Itilima ziwe na Ofisi za TRA ili kuwaondolea wafanyabiashara wenzetu shida ya kufuata huduma katika wilaya nyingine na pia wafanyabiashara tunahitaji elimu ya mara kwa mara kwenye masuala ya kodi” alisema Christina Matulanya Katibu wa TCCIA Simiyu.
“Tunaomba TRA waziangalie upya sheria zao, lakini pia waangalie viwango vya kodi wanavyowakadiria wafanyabiashara ili viendane na hali halisi ya biashara za Watanzania tulio wengi” alisema Davis Mateko Mfanyabiashara kutoka Wilaya ya Busega.
Akizindua kampeni ya Elimu na Usajili kwa walipakodi , Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka ameiomba TRA kutatua changamoto za mashine za kutolea risiti (EFD), huku akitangaza dhamira yake ya kuona biashara zinafanyika saa 24 katika Makao Makuu ya Wilaya na Baadhi ya Vituo (Centres) vikubwa kuiwezesha TRA kukusanya kodi zaidi.
Katika hatua nyingine Mtaka amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani humo kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli la kuzingata maeneo ya wafanyabiashara wadogo wakati wa Ujenzi wa Vituo vya Mabasi na akasisitiza wafanyabiashara wadogo kujisajili ili waweze kupewe kipaumbele vituo hivyo vitakapojengwa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI JUU YA HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/05/tra-kuanzisha-vituo-vya-elimu-na-huduma.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa