Hatimaye suluhu ya mgogoro baina ya mwekezaji wa kampuni ya MWIBA Holdings na wananchi wa vijiji saba vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Makao wilayani Meatu, juu ya utata wa mkataba wa kumiliki ardhi, uanzishwaji wa ranchi ,mahusiano mabovu na kusogezwa kwa alama za mipaka katika makazi ya wananchi imepatikana
Suluhu hiyo imepatikana baada ya kufanyika kikao cha pamoja wilayani Meatu kati ya Kamati ya Siasa ya CCM, Viongozi na Watendaji wa Serikali (Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu), Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Watendaji wa Kampuni ya MWIBA Holdings na Viongozi wa Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makao, ambacho kimeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka
Pande zote mbili (Mwekezaji na wananchi) zimekubaliana kuondoa kesi inayohusu mgogoro huo kwa Msuluhishi Jaji Mstaafu Thomas Mihayo na kurejea tena katika meza ya maridhiano ili kujadili namna ya kuondoa tofauti na dosari zote zilizoonekana awali.
Mtaka ameipongeza Kampuni ya MWIBA Holdings kurejea katika meza ya mariadhiano na wananchi na ameagiza kufanyika mabadiliko katika Menejimenti ya Kampuni hiyo kwa kuwa baadhi ya watendaji wametajwa kuwa chanzo cha migogoro ambayo imekuwa ikiwanufaisha wao wenyewe huku ikichochea uhasama kati ya kampuni hiyo na wananchi
“....Nawaeleza Wakurugenzi, baadhi ya wasaidizi wenu wanawachafua sana, wanatengeneza migogoro na wananchi wetu kwa manufaa yao wenyewe; mkitaka kufanya kazi na sisi chukueni hatua kwa watumishi wenu, tunataka wawekezaji lakini hatuko tayari kuona wananchi wananyanyaswa kwa namna yoyote ile” alisema Mtaka.
Naye Mbunge wa Jimbo la Meatu Salum Khamis amesema nia yake ni kuona wananchi hawabugudhiwi hivyo akatoa rai kuwa maridhiano yatakayofanyika kati ya pande hizo mbili yafanyike kwa umakini sana ili makubaliano yatakayofikiwa yalinde haki za wakazi wa Meatu na yasiwe chanzo cha migogoro.
Wakati huo huo baadhi ya wananchi wamesema mipaka waliyoshiriki kuweka wakati wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Makao, ilitolewa kinyemela na watumishi wakiwemo viongozi wa Jumuiya hiyo kwa kushirikiana na mwekezaji huyo na kusogeza nyuma alama hizo kwa kilomita 10 kutoka eneo la hifadhi kuelekea eneo la makazi ya wananchi
Wananachi hao wamesema kuwa mipaka ambayo imekuwa ikileta migogoro ni mpaka ulioko katika kijiji cha Bulongoja kwenye bikoni namba 314, ambapo walisema kuwa bikoni hiyo iliondolewa na kusogezwa nyuma zaidi ya kilometa 10 kutoka ndani ya hifadhi kuelekea kwenye makazi yao.
Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Katibu Tawala Mkoa, Ndg.Jumanne Sagini amesema atatuma timu ya wataalam Ngazi ya Mkoa ambao watashirikiana na wataalam wa wilaya ya Meatu watakaokwenda kuhakiki mipaka hiyo kwa kuzingatia ramani na kuirejesha ilipokuwa, huku akisisitiza wataalam hao kuzingatia weledi.
Kwa upande wake Mkurugenzi kutoka Makampuni ya Friedkin Game Tracker Safaries na Mwiba Holdings Company Abdulkadir Mohamed amekubali kumaliza mgogoro huo na kufanya mabadiliko ya menejimenti yake ili waweze kufanya uwekezaji wa utalii na mazingira kwa uhuru.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe.Dkt.Titus Kamani amewasa viongozi na watendaji wa Serikali mkoani humo kutekeleza wajibu wao katika kuwaletea wananchi maendeleo na wasiruhusu kwa namna yoyote migogoro ikachukua nafasi kubwa kuliko maendeleo ya wananchi.
Jumuiya Hifadhi ya wanyamapori Makao inaundwa na vijji saba ambavyo ni Makao, Sapa, Mwangudo, Mbushi, Iramba ndogo, Jinamo na Mwabagimu.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa