Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kimeahidi kuwa kiko tayari kuanzisha kituo cha kupima makohozi kwa kutumia panya waliofundishwa kubaini vijidudu vya Ugonjwa wa Kifua Kikuu ambao wanaweza kupima sampuli nyingi kwa wakati mmoja ikilinganishwa na vipimo vya maabara.
Hayo yamebainishwa jana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Mmbaga kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa kudhibiti kifua kikuu ngazi ya jamii uliokuwa ukitekelezwa na mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na shirika lisilo la Kiserikali la Management and Development for Health (MDH), kwa miaka mitatu kuanzia Januari 2018 na unatarajiwa kuhitimishwa Desemba 2020, ambacho kilifanyika jana Mjini Bariadi.
“Tumeona ni muhimu tukaangalia tunavyoweza kutumia teknolojia nyingine kufanya upimaji wa Ugonjwa wa Kifua Kikuu, kwa mfano tumepata fursa ya kushirikiana na wenzetu wa SUA kipindi cha nanenane mwaka huu wamesema wako tayari kutusaidia kuanzisha kituo cha upimaji wa makohozi kwa kutumia panya waliofundishwa,” alisema Mmbaga.
Aidha, Mmbaga amesema mkoa wa Simiyu umeonekana kufanya vizuri katika kuwafikia wagonjwa wa Kifua kikuu ikilinganishwa na mikoa mingine saba ambayo yote inatekeleza mradi wa kudhibiti kifua kikuu ngazi ya jamii chini ya shirika lisilo la Kiserikali la Management and Development for Health (MDH) ambapo umevuka lengo na kuwafikia wananchi kwa asilimia 102.
Pamoja na mafanikio hayo Mmbaga ameelekeza wataalam wafanye tathmini ya malengo yao na waweke malengo mapya yatakayokusudia kuwafikia wananchi wengi wenye uhitaji, ili kupata jamii yenye afya itakayotekeleza kwa vitendo azma na dira ya mkoa ya kuwa mkoa wenye uchumi shindani kwa kutumia rasilimali na fursa zilizopo.
Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za kudhibiti Kifua kikuu na Ukoma, Dkt. Emmanuel John amesema kwa mwaka 2019 Mkoa wa Simiyu ulikuwa na lengo la kuwafikia wagonjwa wa Kifua Kikuu 1631 ambapo mpaka kufikia mwezi Desemba 2019 wagonjwa takribani 1673 walikuwa wamefikiwa sawa na asilimia 102 ya lengo.
Dkt. John ameongeza kuwa katika wagonjwa waliokuwa wameanzishiwa matibabu kwa mwaka 2018/2019 asilimia 72 waliweza kupona kabisa, huku akibainisha kuwa katika asilimia 28 baadhi yao walifariki, baadhi walipotea katika mifumo ya matibabu (watoro); huku akiweka bayana kuwa kwa mwaka 2020, lengo la Mkoa ni kuwafikia wagonjwa 1779.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Simiyu, Dkt. Khamis Kulemba amesema kuwa wataalam wa afya ngazi ya mkoa na halmashauri watahakikisha wanafanya marejeo ya malengo yao yaweze kuakisi hali halisi ya mahitaji ya jamii ili wananchi wengi waweze kufikiwa na huduma za upimaji na matibabu ya Kifua Kikuu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Management and Development for Health (MDH), Bw. Eliamin Busara amesema katika awamu ijayo shirika hilo linatarajia kujikita zaidi katika mpango wa Kifua Kikuu na uboreshaji wa huduma za mama na mtoto hususani katika kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Wakati huo huo Busara ametoa wito kwa Serikali kupitia halmashauri kuwa na mipango ya namna ya kuendeleza huduma zilizokuwa zikitolewa kwa wananchi kupitia mradi huo ili huduma za afya zisitetereke hususani katika upimaji na matibabu ya Kifua Kikuu.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-http://simiyuregion.blogspot.com/2020/08/blog-post_5.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa