Mkoa wa Simiyu umewahakikishia wadau wote wa Maonesho ya Nanenane upatikanaji wa miundombinu yote muhimu hususani miundombinu ya maji, umeme na barabara katika Uwanja wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Mashariki uliopo eneo la Nyakabindi Mjini Bariadi, ambapo Mkoa huo utakuwa mwenyeji wa Maonesho hayo Kitaifa mwaka 2018.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini alipokutana na Kamati ya Maadalizi ya Maonesho Nanenane kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambao walitembelea uwanja huo na kupewa eneo ambalo litatumika na wizara hiyo kuonesha shughuli zake.
Sagini amesema viongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na viongozi wa Taasisi nyingine za Serikali wameshafanya mazungumzo na kuweka mipango ya namna kila Taasisi itakavyoshiriki katika kuhakikisha miondombinu ya maji, umeme na barabara inawekwa vizuri ili kufanikisha Maonesho hayo
“Tumeshazungumza na TANESCO na wako tayari kuteremsha Transifoma kwenye eneo lile ili tupate umeme, tumezungumza na Mamlaka za Maji ili tupate fedha za kuchimba kisima kirefu cha maji ya kutosheleza wadau wetu na kuhusu barabara tumezungumza na TANROADS na TARURA, tunatarajia wiki mbili zijazo mambo yatakuwa tofauti pale” alisema Sagini.
Aidha, Sagini amesema pamoja na kushughulikia miundombinu, Mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ambayo inaunda Kanda ya Nanenane ya Ziwa Mashariki, imeshafanya vikao vya wataalam na kuweka mipango mbalimbali ya kufanikisha maonesho hayo na akabainisha kuwa Mei 17, kitafanyika kikao kikuu cha maamuzi kwa lengo la kufikia maamuzi ya nini kinafanyika kwa wakati gani na nani atakayefanya.
Wakizungumza mara baada ya kutembelea eneo la Uwanja wa Nanenane Kanda ya Ziwa Mashariki, wawakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na kupongeza uongozi wa mkoa kwa juhudi zinazofanyika, kuridhishwa na hali ya maandalizi ya uwanja wameshauri kasi ya maandalizi iongezeke ili kuendana na muda uliobaki kuelekea maonesho.
“Viwanja tumeviona viko mahali pazuri na eneo tumepewa, kwa muda uliobaki tunashauri waongeze speed(kasi) wameshaanza kugawa maeneo kwa wadau na wameshaanza kuyasafisha, lakini waharakishe kuweka miundombinu ya maji,barabara na umeme” alisema Merry Yongolo Mratibu wa Maonesho ya Nanenane Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
“Natoa pongezi kwa Mkoa wa Simiyu kwa kukubali kuwa mwenyeji wa Nanenane mwaka huu hii ni fursa waitumie, sisi kama wizara pia tunaona hii ni fursa hasa katika kukutana na wafugaji na wavuvi na kutatua changamoto zinazowakabili; ili tuweze kufanikisha maonesho haya maandalizi ya mapema ni muhimu sana alisema Dkt. Khamis Mkuli kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Naye Mkurugenzi wa shughuli za utafiti Kanda ya Ziwa Moses Ngendelo amesema katika maonesho hayo wanatarajia kuonesha teknolojia mpya ambazo zitawasaidia wafugaji, wakulima na wavuvi kuongeza tija katika uzalishaji, hivyo akatoa wito kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kushiriki maonesho hayo ili waweze kuona teknolojia hizo.
Hivi karibuni Wizara ya kilimo imetangaza Kanda Mpya ya Maonesho ya Nanenane ijulikanayo kama Kanda ya Ziwa Mashariki, ambayo inajumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga na Uwanja utakaotumika kwa ajili ya Maonesho hayo uko Eneo la Nyakabindi Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/05/simiyu-yawahakikishia-wadau-upatikanaji.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa