Mkoa wa Simiyu umepokea jumla ya vitabu 174,188 awamu ya kwanza kwa masomo ya Kiingereza na Hisabati, vyenye thamani ya takribani shilingi milioni 348 kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la nne, ambavyo ni sawa na uwiano wa mwanafunzi mmoja kwa kitabu kimoja.
Akizungumza na viongozi , baadhi ya walimu na wanafunzi wa mkoa wa Simiyu kabla ya kukabidhi vitabu vitabu hivyo kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka Julai 05 jioni mjini Bariadi, Mwakilishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Bw. Didas Hamsini, amesema Taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha vifaa vyote vya kielimu ikiwemo vitabu, vifaa vya maabara na vifaa vingine vinavyohitajika vinapatikana.
Amesema utoaji wa vitabu 29,003 kwa kila somo kwa wanafunzi wa darasa la nne Mkoani Simiyu ni sehemu ya utekelezaji wa elimu bila malipo, huku akibainisha kuwa Taasisi ya Elimu inatarajia kuzalisha vitabu 681, 527 kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la nne nchi nzima.
Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Julius Nestory amesema wamepokea vitabu awamu ya kwanza kwa masomo ya kiingereza na hisabati kwa uwiano wa kitabu kimoja mwanafunzi mmoja, huku akibainisha kuwa vitabu vilivyobaki vinatarajiwa kuletwa tena wiki ya kuanzia tarehe 16 Julai, 2018 na akawataka walimu na wanafunzi kuvitumia vitabu hivyo kama ilivyokusudiwa.
“Naishukuru sana Serikali kwa kutoa vitabu hivi hadi sasa tuna wanafunzi 53, 187 darasa wa nne na vitabu tulivyopokea kwa awamu hii kwa masomo ya Hisabati na Kiingereza, kila mwanafunzi wa Mkoa wa Simiyu atapata kitabu cha kwake, kwa masomo manne yanayobaki tumeahidiwa kuwa baada ya majuma mawili vitakuwa vimefika” alisema Afisa Elimu Mkoa.
Kwa upande wao wanafunzi wa mkoa wa Simiyu wameishukuru Serikali kwa kuwaletea vitabu, hivyo ambavyo wanaamini vitawasaidia kujisomea na kuinua ufaulu hatimaye kuufikisha mkoa huo katika mikoa kumi bora inayofanya vizuri kitaaluma.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuwaleta hivi vitabu, tunaamini vitawasaidia wadogo zetu wa darasa la nne kujifunza na kuongeza ufaulu na siku moja mkoa wetu na sisi utakuwa kati ya mikoa bora inayofanya vizuri kitaaluma “ alisema Liku Malisha mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Somanda A.
Mbunge wa Itilima Mhe. Njalu Silanga ameishukuru Serikali kwa kutoa vitabu hivyo na akatoa wito kwa walimu na wanafunzi mkoani humo kuhakikisha kuwa vitabu hivyo vinawezesha kuongeza ufaulu kwa kuwa mkoa huo umeshajipanga kutokomeza ujinga na kuwa mkoa kiongozi kielimu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutimiza ahadi yake na kujibu kilio cha muda mrefu cha wazazi, walimu na wanafunzi juu ya changamoto ya ukosefu wa vitabu wa darasa la nne.
Ameongeza kuwa vitabu hivyo vitausaidia mkoa wa Simiyu kufikia malengo yake katika kuongeza ufaulu na kuboresha Sekta ya Elimu, ambapo amebainisha kuwa kupata vitabu hivyo, kupata walimu, kukamilisha miundombinu na mwamko wa wazazi kuchangia chakula watoto wao shuleni kutaufanya mkoa huo kushindana kielimu katika miaka ya mbeleni.
Katika hatua nyingine Mhe. Mtaka amewataka walimu mkoani humo kuwafundisha kwa moyo, wanafunzi kuvitumia vema vitabu hivyo na wazazi kuwafuatilia watoto wao katika masomo ili wanafunzi waweze kufanya vizuri, kwa kuwa ufaulu wa mwanafunzi hutegemea ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi na wazazi.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Somanda A, mara baada ya makabidhiano ya vitabu vya Darasa la nne mkoani humo na Mwakilishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Bw. Didas Hamsini, yaliyofanyika Julai 05, 2018 katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Bariadi.
Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius Nestory akihojiwa na waandishi wa habari baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka Mtaka kukabidhiwa vitabu vya Darasa la nne na Mwakilishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Bw. Didas Hamsini, katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Bariadi Julai 05, 2018.
Mbunge wa Itilima Mkoani Simiyu, Mhe. Njalu Silanga akihojiwa na waandishi wa habari baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka Mtaka kukabidhiwa vitabu vya Darasa la nne na Mwakilishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Bw. Didas Hamsini, katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Bariadi Julai 05, 2018.
Abdallah Twalib Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Somanda A, akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kukabidhiwa vitabu vya Darasa la nne mkoani humo na Mwakilishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Bw. Didas Hamsini, katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Bariadi
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa