Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema Sekretarieti ya Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani Simiyu zimekisia kutumia jumla ya shilingi 175,260,331/= kwa ajili ya miradi ya maendeleo, mishahara na matumizi mengineyo.
Sagini ameyasema hayo Machi 15, 2019 wakati akiwasilisha rasimu ya Mapendekezo ya Mpango wa Bajeti ya mwaka 2019/2020 katika kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa(RCC) kilichofanyika Mjini Bariadi.
Amesema katika kiasi tajwa, shilingi 41,960,264,000/= zitatumika katika miradi ya maendeleo, shilingi 18,522,914,000/= kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 114,777,153,000/= kwa ajili ya mishahara.
Aidha, Sagini amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekadiria kukusanya jumla ya shilingi 13, 004,878,000/= kutokana na vyanzo vyake vya ndani, ambapo kati ya hizo shilingi 4,745,216,000/= sawa na asilimia 36.5 zitatumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shilingi 8,259,662,000/= zitatumika kwa ajili ya uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ameongeza kuwa mpango wa bajeti umezingatia masuala muhimu kwa mkoa ambayo ni kusimamia na kudumisha masuala ya amani na utulivu, kuimarisha utawala bora na uwajibikaji kwa kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika kwa amani na utulivu, kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje, kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu na maji hususani kwa wananchi waishio vijijini.
Masuala mengine ni Kuzisimamia Halmashauri ili kubuni, kuandaa maandiko na kufuatilia utekelezajiwa miradi ya maendeleo ya kuongeza kipato cha halmashauri, kuimarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi,kuendeleza ujenzi wa ofisi, nyumba za viongozi na hospitali za wilaya Itilima, Bariadi na Busega.
Pamoja na hayo mpango huu umezingatia kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi, kuimarisha usimamizi wa mapato ya ndani na kuibua vyanzo vipya, kuhuisha mipango mkakati ya mkoa na halmashauri na kuanza kutekeleza dhana ya kuimarisha utendaji wa kuongeza tija katika utekelezaji wa kazi na miradi ya kiuchumi.
Awali akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.John Magufuli kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Hospitali tatu za Wilaya mkoani hapa.
“Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na pia tumepata shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya ya Bariadi, Busega na Itilima” alisema Mtaka .
Katika hatua nyingine Mtaka amewapongeza Wabunge wa Mkoa huu kwa namna wanavyoshiriki katika kuhimiza shughuli za maendeleo huku akiwataka viongozi wote kuwaunga mkono ikiwa ni pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani humo kujipambanua katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo itawasaidia kuongeza kipato, huku ikiipongeza wilaya ya Maswa kwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa kiwanda cha vifungashio na upanuzi wa kiwanda cha chaki miradi ambayo itakuwa chanzo cha uhakika cha mapato kwa Halmashauri.
Wajumbe mbalimbali waliohudhuria katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa waliunga mkono mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2019/2020 huku wakisisitiza Halmashauri kuwa na miradi ya kimkakati ili ziweze kupata vyanzo vipya vya mapato na wananchi kujiunga na bima ya afya ili kujihakikishia huduma za matibabu.
“Ninashauri Halmashauri ziwe na mradi ya kimkakati itakayoziongezea mapato yao ya ndani kama ilivyofanya Maswa ambayo inaenda kuwa na viwanda vikubwa viwili cha chaki na kiwanda cha vifungashio, tena hasa nashauri kasi iongezeke hapa Bariadi ambapo ndiyo sura ya Mkoa”alisema Gungu Silanga Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa,kupitia Simiyu.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa naunga mkono suala la kuhamasisha wananchi wetu kujiunga na Bima ya Afya tena natoa wito kwa viongozi wenzangu tuwe mabalozi kwa wananchi wetu tuwaelimishe na kuwahamasisha kujiunga na Bima ya Afya ili wawe na uhakika wa kupata matibabu”alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mhe. Pius Machungwa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/03/simiyu-yakisiwa-kutumia-shilingi.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa