Mkoa wa Simiyu umeidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 13.1 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na miradi ya maendeleo katika bajeti ya mwaka 2018/2019.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS)'Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. Albert Kent wakati akiwasilisha taarifa katika Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa, kilichofanyika Desemba 14, 2018 Mjini Bariadi.
Kent amesema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 11.461 zimeidhinishwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara kutoka katika mfuko wa barabara na shilingi bilioni 1.595 utekelezaji wa miradi 12 ya maendeleo yenye urefu wa kilometa 78.2.
Aidha, Kent amezungumzia maendeleo ya ujenzi wa daraja la mto Sibiti na kubainisha kuwa ujenzi wake umefikia asilimia 85 na jitihada zinaendelea kufanyika, ili ifikapo mwezi Machi, 2019 liwe limekamilika kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli mwezi Septemba, 2018 wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo.
Naye Mratibu wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Mhandisi. Salvatory Yambi amesema katika bajeti ya mwaka 2018/2019 Mkoa wa Simiyu umeidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 5.4 na kubainisha kuwa hadi sasa TARURA inaendelea kutekeleza miradi 29 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.6 ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Awali akifungua kikao cha Bodi ya Barabara kwa niaba ya Mwenyekiti wa kikao hicho na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amepongeza TANROADS na TARURA kwa kazi kubwa wanayoifanya mkoani humo, hususani katika kusimamia ujenzi na matengenezo barabara hali iliyochangia kuufungua mkoa na kuchochea kukua kwa uchumi.
Akichangia hoja katika kikao hicho, Mbunge wa Bariadi, Mhe. Andrew Chenge ameshauri kuwepo na uhusiano wa karibu kati ya TARURA na Halmashauri hususani katika maandalizi ya Bajeti, ili vipaumbele vya TARURA vizingatie vipaumbele vya Halmashauri ambao ndio wanaokutana na wananchi moja kwa moja na kujua mahitaji yao.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa Simiyu, Jumanne Sagini ametoa wito kwa Wakurugenzi wa halamshauri kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara ambazo haziko chini ya TARURA hususani katika kipindi hiki cha maandalizi ya bajeti.
Katika kikao hiki pia wajumbe mbalimbali walipata nafasi ya kuchangia hoja ambazo zililenga kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja, masuala yote ambayo Mhandisi Kent alieleza kuwa yatafanyiwa kazi na yanayohitaji hatua zaidi kutoka katika wizara yenye dhamana yatafikishwa.
"Nashauri wananchi washirikishwe katika zoezi la uwekaji wa alama za vivuko wakati barabara ya Maswa-Bariadi itakapokamilika ili viwekwe mahali penye uhitaji" Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe
"Ili daraja la Sibiti liweze kuleta tija zaidi tunaomba TANROADS iandae mpango wa dharura wa kujenga daraja la Mto Itembe ili kuwaondolea adha wananchi waweze kuvuka kutoka eneo moja kwenda kwingine pindi mvua zinaponyesha." Mhe. Leah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum CCM.
Mwenyekiti Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mhe. Robert Lweyo ameshauri ijengwe round about (mzunguko) Mjini Bariadi katika makutano ya barabara ya Ngulyati-Bariadi, Lamadi- Bariadi na Maswa-Bariadi, jambo ambalo Mhandisi Kent aliahidi kuliandikia barua na na kuliwasilisha katika wizara yenye dhamana na ujenzi.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/12/simiyu-yaidhinishiwa-bilioni-13.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa