Mkoa wa Simiyu umeweza kusajili jumla ya watoto 337,662 kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita sawa na asilimia 91.7 ya watoto waliotarajiwa kusajiliwa, chini ya mpango wa Usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano, unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Katiba na Sheria (RITA), Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na wadau wengine..
Akizungumza katika kikao cha Tathmini kuhusu utekelezaji wa mpango wa usajili wa vizazi kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bi. Emmy Hudson amesema kabla ya mpango huo Mkoa wa Simiyu ulikuwa na usajili wa chini kwa asilimia 5
“Kwa mujibu wa takwimu mpaka sasa Mpango huu katika Mkoa wa Simiyu umeweza kusajili watoto 337,662 ambao ni sawa na asilimia 91.7 ya watoto wote waliotarajiwa kusajiliwa...hii ni dhahiri kuwa ni mafanikio makubwa kwani kabla ya kuanza kwa mpango kulikuwa na asilimia 5 tu ya watoto waliokuwa wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa”...Alisema
Aidha, Hudson alisema kuwa mbali na mafanikio hayo yaliyopatikana ni lazima kila Halmashauri kuendeleza mpango huo kwani bila hivyo watakuwa wanarudisha nyuma jitihada za serikali la kufikia usajili wa watoto wa miaka mitano kuwa asilimia 100.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Jumanne Sagini alisema kuwa pamoja na mkoa huo kufikia asilimia hiyo 91 ,ni vema sasa halmashauri zikajitahidi kufikisha lengo la usajili kwa asilimia 100.
Sagini pia alizitaka Halmashauri zote ziweke mipango mikakati ya namna ya kuendeleza usajili huo wa watoto chini ya miaka mitano na kuweka katika mipango ya bajeti kwani hazitaweza kufadhiliwa miaka yote.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amesema kuwa zoezi la usajili katika wilaya yake liliendeshwa vizuri ingawa kulikuwa na changamoto kadhaa ambazo zilitatuliwa kwa kadri zoezi la usajili lilivyokuwa likiendelea na kuiwezesha wilaya hiyo kufanya vizuri pia.
Kiswaga ameeleza kuwa kupitia matokeo hayo ya mpango wa usajili ndani ya miezi mitatu utasaidia kuchochea maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa ujumla, kutokana na kuwepo kwa takwimu na taarifa za watoto wa chini ya mikaa mitano zitakazotumika kupanga mipango ijayo ya maendeleo ngazi zote.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian Manoza amewapongeza RITA kwa kusimamia mpango huo ambao utasaidia kuboresha na kupanga mikakati ya Serikali hususani katika sekta ya afya kwa kuwezesha upatikanaji wa takwimu za watoto wenye umri chini ya miaka mitano .
“Naamini kuwa kwa sasa tutaweza kupanga mipango yetu vema kwani mwanzoni tulikuwa tunapata shida sana wakati wa kupanga mipango ya afya, hususani katika ugawaji wa chanjo kwa watoto, kutokana na kukosa takwimu sahihi za watoto...”Alisema Manoza
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho cha miezi mitatu walikusudia kuwafikia watoto 68,000 lakini waliofikiwa ni 63,000 kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo mvua ambayo ilisababisha baadhi ya maeneo kutokufikika, huku akibainisha mkakati wa kuendeleza usajili na kuongeza wigo wa kuwafikia wananchi kwa karibu kupitia Ofisi za Vijiji.
Mpango wa Usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano ulianza kutekelezwa Mwezi Machi 14 mwaka huu mkoani Simiyu, ambapo kwa mikoa ya Mara na Simiyu, ulizinduliwa rasmi na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi Mjini Musoma Mkoani Mara Machi 20, 2018.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI ZA KIKAO HIKI FUGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/07/simiyu-yafanikiwa-kusajili-na-kutoa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa