Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally amesema Mkoa wa Simiyu ni mkoa wa kwanza katika utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mshikamano kati ya Serikali na Chama Tawala.
Dkt. Bashiru amesema hayo wakati akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi katika Kilele cha Maonesho ya Nane nane Kitaifa mwaka 2018 Mkoani Simiyu, Uwanja wa Nyakabindi, Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
“ Simiyu ni Mkoa wa Kwanza kwa Tanzania Bara katika Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, matokeo tunayoyaona, haya yanayotufurahisha chanzo chake ni mshikamano baina ya Viongozi wa Chama na Serikali katika Mkoa” alisema Dkt. Bashiru.
Wakati huo Dkt. Bashiru ameitaja mikoa mitatu ikiongozwa na Simiyu ambayo inafanya vizuri katika Utekelezaji wa Ilani ya CCM kuwa ni pamoja na Singida, Dodoma na Pwani, huku akieleza kuwa katika mikoa hiyo viongozi na watendaji wa Chama wanafanya kazi kwa kushirikiana katika shida na raha.
Aidha, ameitaja mikoa minne ambayo haifanyi vizuri kuwa ni Mara, Arusha, Mbeya na Dar es Salaam na akawataka viongozi wa Chama na Serikali katika mikoa hiyo kujirekebisha ili waweze kufanya kazi kwa kushirikiana.
Amesema Chama kimeumizwa sana na makundi na kinapata tabu pale ambapo viongozi wa Chama na Serikali hawana mtazamo mmoja, hivyo amewataka viongozi wa mikoa ya Mara, Mbeya, Arusha na Dar es Salaam kushikamana na kuwa kitu kimoja ili waweze kuwatumikia wananchi ipasavyo.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema uhusiano kati ya Chama na Serikali kwa mkoa huo kuanzia ngazi ya Kijiji na Tawi hadi mkoa uko vizuri na akimhakikishia Katibu Mkuu wa CCM kuwa mshikamano baina yao utaendelea kuimarishwa.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa