Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umemtunuku cheti cha shukrani aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini ikiwa ni kutambua mchango wake katika kukuza sekta ya elimu katika Mkoa wa Simiyu wakati wa uongozi wake, kabla ya kuteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM kuwa Mgombe wa Ubunge katika Jimbo la Butiama mkoani Mara.
Akimkabidhi cheti hicho Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga amesema uongozi umetoa cheti hicho kama alama katika kushukuru na kuthamini mchango wa Ndugu Sagini katika maendeleo ya sekta ya elimu na mkoa wa Simiyu kwa ujumla.
“Tunakutakia kila la heri na tunaahidi kuwa tutaendelea kuishi ndoto na dhamira ulizoshiriki kuzitengeneza ukiwa na Mkuu wetu wa mkoa Mhe. Anthony Mtaka ili kuhakikisha elimu inasonga mbele na mkoa wa Simiyu unakuwa nambari moja katika kila eneo,” alisema Bi. Mmbaga.
Akipokea cheti hicho aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amewashukuru viongozi wa mkoa kwa kutambua mchango wake huku akibainisha kuwa wakati wa uongozi wake kama msimamizi mkuu wa utekelezaji wa yale waliyokuwa wakikubaliana alipata ushirikiano kutoka kwa viongozi na watendaji kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya.
“ Ninawashukuru sana viongozi wa mkoa mkiongozwa na kiongozi Mkuu Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa kutambua mchango wangu, nimefarijika kuona mimi nilipotoka Simiyu kwenda kwenye shughuli za kisiasa, yale tuliyopanga kama mkoa yametimia maana mwaka juzi tulishika nafasi ya kumi, mwaka jana tukabaki hapo lakini mwaka huu nasikia mmeshika nafasi ya tatu hongereni sana, natamani lengo la kushika nafasi ya kwanza litimie,” alisema Sagini.
Aidha, Sagini ameomba Mkoa wa Simiyu ukubali kuwa marafiki wa Wilaya ya Butiama na Mkoa wa Mara kwa ujumla, ili kuendeleza ushirikiano kati ya wilaya na mikoa jirani; huku akitoa wito kwa viongozi wa mkoa wa Simiyu kukubali na kutoa ushirikiano pale watu wa Butiama na Mara watakapohitaji kujifunza na kupata uzoefu kutoka kwao.
Jumanne Sagini aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2016 na aliachia nafasi hiyo Julai 03 mwaka huu baada ya kuanza kushiriki mchakato wa kugombea ubunge katika Jimbo la Butiama ambapo amepewa ridhaa na Chama Cha Mapinduzi kupeperusha bendera ya Chama hicho katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/08/simiyu-wamtunuku-cheti-aliyekuwa-ras.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa