Serikali imetoa jumla ya shilingi 2,327,259,225 kwa walengwa wa TASAF III awamu ya pili wapatao 28984 kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini katika kipindi cha mwezi Julai hadi Oktoba mwaka 2020 katika vijiji 376 mkoani Simiyu.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa TASAF mkoa wa Simiyu, Bw. Nyasilu Ndulu Septemba 23, 2020 wakati wa zoezi la uhawilishaji fedha kwa walengwa wa TASAF wa kijiji cha Mwamishali wilayani Meatu.
“Fedha za walengwa tulizopokea ni shilingi 2,327,259,225 na hizi ni fedha za awamu mbili, mwezi Julai-Agosti na Septemba-Oktoba na zinalipwa kwa awamu moja; fedha hizi zimefika kipindi muafaka cha maandalizi ya msimu wa kilimo nawashauri wazitumie vema katika maandalizi ya shughuli za kilimo lakini wajiwekee utaratibu wa kuwekeza kwenye shughuli za uzalishaji,” alisema Nyasilu.
Akizungumza na walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Mwamishali Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Miriam Mmbaga ametoa rai kwa walengwa wao kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha hiyo ya ruzuku wanayopata ili waweze kufikia malengo yao.
“Ninawasihi muendelee kujiamini na kila mmoja atambue kuwa anaweza, uwezeshaji ndiyo huu umeletwa na serikali hivyo ni kila mmoja akijiamini kuwa atafanikiwa kupitia kazi anayofanya atafanikiwa, kama mtu anafuga kuku, mbuzi, au ng’ombe akiwatunza vizuri akisaidiwa na wataalam wa halmashauri mtakuza vipato vyenu na mtafikia malengo yenu,” alisema Mmbaga.
Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bi. Kija Kayenze amesema ruzuku ya fedha zilitolewa kwa walengwa wa TASAF zimefika katika kipindi muafaka, ambapo msimu wa kilimo unatarajiwa kufunguliwa Oktoba Mosi; huku akitoa wito kwa walengwa kutumia fedha hizo katika uandaaji wa mashamba, ununuzi wa mbegu bora ili waweze kupata mavuno bora.
Nao baadhi ya walengwa wa TASAF wameishukuru Serikali kwa kutoa ruzuku ya fedha ambazo zimewasaidia kuanzisha miradi midogo midogo hususani katika kilimo, ufugaji na ujasirimali ambayo inawawezesha kupata mahitaji yao ya kila siku na kuweka akiba kwa ajili ya baadaye.
“Naishukuru serikali kutusaidia kupitia TASAF, nilikuwa nafanya vibarua kupata hela ya matumizi na kuwanunulia wanangu mahitaji ya shule, lakini nilipoanza kupata hela za TASAF nikawa nazitunza baadaye nikanunua ng’ombe wawili ambao sasa hivi wamezaa, nategemea kuwauza wawili ili ninunue bati za kuezeka nyumba yangu na kupata mtaji,” alisema Sikitu Zengo mkazi wa Kijiji cha Mwamishali wilayani Meatu.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2020/09/zaidi-ya-shilingi-bilioni-23-zatolewa.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa