Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kujenga jengo la wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, ili hospitali hiyo iweze kutoa huduma za kulaza wanawake na watoto.
Waziri Ummy ameyasema hayo Julai 16, 2019 wakati akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la maabara, jengo la upasuaji ambalo pia litakuwa na huduma za mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi.
Amesema wagonjwa wengi ni wanawake na watoto wadogo hivyo ni vema wakajengewa wodi huku akibainisha pia kuwa Serikali imeshatoa shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la maabara na jengo la upasuaji ambalo pia litakuwa na huduma za mionzi unaotarajia kukamilika mwezi Oktoba 2019.
“Tulianza na ujenzi wa jengo la OPD, na awamu ya pili namshukuru Mhe. Rais ametoa shilingi bilioni 5.7 kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya ujenzi wa jengo la maabara, jengo la upasuaji ambalo pia litakuwa na huduma za mionzi”
“Sasa hivi tuna shilingi bilioni 2.2 kwenye akaunti ya Hospitali na tutaanza kujenga jengo la mama na mtoto, ili tuanze kulaza wagonjwa maana hata ukiangalia wagonjwa wengi ni wanawake na watoto wadogo, hili la wodi za watu wengine nalo pia tunalibeba” alisema Waziri Ummy.
Aidha, Mhe. Waziri amepongeza wakala wa Majengo TBA mkoa wa Simiyu kwa kutekeleza miradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa huku akimtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kurejesha fedha zilizokatwa kodi(withholding tax) wakati akilipa TBA gharama za ujenzi, ili zifanye kazi ya ujenzi maana TBA kama Taasisi ya Umma haipaswi kukatwa fedha hizo.
Naye Meneja wa TBA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. Likimaitare Naunga amesema ikiwa fedha kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 204 zilizokatwa kama kodi “Withholding Tax” zikirejeshwa zitasaidia kununua vifaa vya kukamilishia majengo hayo.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru Serikali kwa kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, ambayo yataendelea kuboresha huduma kwa wananchi, ambapo pia ameishukuru wizara ya afya kwa kuendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa majengo hayo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo amesema CCM kama wasimamizi wa utekelezaji wa Ilani wanashukuru kwa namna Serikali inavyotekeleza ilani katika kuboresha huduma za afya Mkoani Simiyu na ameahidi kuwa wataendela kufuatilia na kusimamia kwa karibu ili kuhakikisha huduma bora zinatolewa.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/07/serikali-yatoa-shilingi-bilioni-22.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa