Serikali mkoani Simiyu imeomba kuwepo kwa kikundi cha ulinzi cha kijeshi katika Wilaya ya Busega ili kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu ikiwemo uvuvi haramu na kuwezesha ufugaji wa samaki ndani ya Ziwa Victoria kufanyika kwa usalama.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka wakati wa Hafla ya kumpongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini, Jenerali Venance Mabeyo iliyoandaliwa na ndugu zake kijijini kwao Yitimwila ‘A’ katika Kata ya Kiloleri Wilayani Busega.
“Tumepata changamoto nyingi sana kwenye ziwa, matukio mengi ya kihalifu liliwemo la uvuvi haramu , sisi kama mkoa tulikuja na wazo kwamba tungehitaji tupate ‘detouch’ moja eneo la Ziwa ili ukanda huu baada ya kufanya kazi kubwa ya kuchoma makokoro ya wananchi, tuwapeleke kwenye uvuvi wa kisasa hususani ufugaji wa samaki ziwani, jambo ambalo Mheshimiwa Rais analipa kipaumbele sana; na namna pekee ya kufanya ufugaji ule wa samaki ziwani, suala la ulinzi na usalama ni muhimu sana; ” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amesema pamoja na kufanya ufugaji wa samaki katika Ziwa Victoria, Serikali ya Mkoa imefanya makubaliano na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF kuwawezesha wananchi wa Busega kufanya kilimo cha Umwagiliaji kwa kutumia maji ya ziwa hilo ambayo ni ya uhakika.
“Tumeongea na NSSF kwa ajili ya kuanzisha mradi ambao hautazidi bilioni moja, tutaleta mbegu za aina ya nyanya na pilipili zinazotakiwa ili wananchi wa Busega wazalishe kwa wingi. Hatutakuwa tayari kuona wananchi wanalima nyanya na kuuza ndoo moja shilingi 500, tumepanga kuanzisha mradi wa kuzalisha ‘chill sauce’ na ‘tomato source’ .”alisema Mtaka.
Ameongeza kuwa Wataalam wa Wilaya na Mkoa kwa kushirikiana na Wataalam wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji , Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru wanafanya upembuzi yakinifu kuona namna miundombinu ya umwagiliaji itakavyojengwa ili kuwawezesha wananchi wa Busega kulima muda wote kupitia kilimo cha Umwagiliaji badala ya kutegemea mvua.
Mtaka amesema Serikali mkoani Simiyu imedhamiria kuhakikisha katika kipindi cha miaka mitatu ijayo Mkoautapunguza kasi ya uingizaji wa bidhaa kutoka nje na badala yake wananchi wake watazalisha na kutumia bidhaa zao wenyewe, hivyo ameomba Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuona namna ya kuweka vituo vya kuuza zana za kilimo katika maeneo ya kanda ya Ziwa ili wananchi wapate zana bora za kisasa zitakazowasaidia kulima kisasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi , Jenerali Venance Mabeyo amewataka wananchi wa Busega kubadili mtazamo wao na kutumia maji ya ziwa Victoria kwa manufaa yao kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili wasikumbwe na tatizo la upungufu wa chakula kunapotokea ukame.
Kuhusu suala la ulinzi katika Ziwa Victoria amesema ombi la Serikali ya Mkoa la kuwa na kikundi cha Ulinzi, viongozi watalitafakari kuona namna ya kulishughulikia na akaeleza kuwa tayari Jeshi limeweka kikundi kidogo cha kiulinzi kutoka Jeshi la wanamaji, lakini kutokana na ukubwa wa Ziwa Victoria kikundi hicho hakiwezi kuhimili kufanya doria maeneo yote na akaahidi kukiimarisha zaidi.
Jenerali Mabeyo pia amewaasa vijana wa Busega na mkoa wa Simiyu kwa ujumla kujiunga katika vikundi ili Serikali iwasaidie kutafuta mitaji ya kujishughulisha na Kilimo, uvuvi na ufugaji badala ya kukimbilia JKT tu, japo amesema kwenda kwao JKT kunaweza kuwasaidia kupata stadi mbalimbali za maisha.
Naye Mwakilishi wa Baraza la Wazee wa Wilaya ya Busega, Bibi. Perazia Ndaki akisoma risala ya wazee kwa Mkuu wa majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo amemuomba Mkuu huyo wa majeshi kuona uwezekano wa kuanzisha Kambi ya jeshi la Kujenga Taifa(JKT) katika mikoa ya kanda ya Ziwa na hususani Mkoa wa Simiyu ili kuwasaidia vijana wengi kujiunga na kupata stadi mbalimbali zitakazowasaidia kujiajiri katika uvuvi, kilimo na ufugaji.
Mbunge wa Jimbo la Busega, Mhe.Raphael Chegeni amemuhakikishia Mkuu huyo wa majeshi kuwa endapo ombi la kuanzisha kambi katika Mkoa wa Simiyu litaridhiwa, Wilaya ya Busega itatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kambi hiyo ambalo lipo tayari.
Sanjali na hilo viongozi mbalimbali wa dini walioshiriki katika hafla ya kumpongeza Mkuu huyo wa Majeshi, wamesisitiza wananchi kuwaombea yeye pamoja na viongozi wote wa Serikali wa ngazi zote ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika kuwatumikia wananchi.
Hafla ya kumpongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo imefanyika kwa ajili ya ndugu zake kumpongeza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli katika nafasi hiyo, ambapo ilitanguliwa na ibada ya shukrani iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Ilumya Wilayani Busega, Jimbo la Shinyanga.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa