Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa amesema Serikali inatarajia kuzindua rasmi mfuko wa watu wenye ulemavu ambao utakuwa ukishughulikia masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu ikiwemo kutoa ruzuku kwa vyama vya watu wenye ulemavu.
Mhe. Ikupa ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali na watu wenye ulemavu wakati akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo, Februari 26,2019.
Amesema taratibu zote zimekamilika na sasa iko katika hatua za mwisho ili mfuko huo uweze kuzinduliwa huku akibainisha kuwa Baraza la Ushauri kwa watu wenye Ulemavu Taifa nalo litazinduliwa hivi karibuni kwa kuwa tayari Mwenyekiti wa Baraza hilo ameshateuliwa na Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
“Tayari tumeshapata Mwenyekiti wa lile Baraza la Ushauri kwa watu wenye ulemavu ambaye ameteuliwa na Mhe. Rais na tunaamini muda si mrefu lile baraza litazinduliwa na litaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria” alisema Naibu Waziri Ikupa.
Katika hatua nyingine Mhe. Ikupa amepongeza viongozi wa Wilaya ya Meatu kwa namna wanavyoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu na wakati huo huo akawapongeza watu wenye ulemavu wilayani humo kutumia vema fedha za mikopo wanazopata kutokana asilimia mbili za mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kuanzisha shughuli za ujasiriamali.
Aidha, ametoa wito kwa watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo hiyo ambayo haina riba ili waweze kuanzisha shughuli za ujasiriamali zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani amesema Halmashauri ya Wilaya hiyo imetenga takribani shilingi milioni Sabini kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi watu wenye ulemavu na akatoa wito kwao kujitokeza kuomba mikopo ili iwasaidie kuanzisha shughuli za kuwaingizia kipato.
Kwa upande wao watu wenye ulemavu wameiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kusaidia katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na ukosefu vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu na kutengeneza mazingira wezeshi shuleni kwa wanafunzi wenye ulemavu.
“ Tunaomba Serikali yetu kwa kushirikiana na wadau itusaidie kupata nyenzo saidizi kama fimbo nyeupe kwa wasioona, viungo bandia na baiskeli za miguu mitatu kwa walemavu wa viungo” alisema Ndimila Luyoja Katibu wa SHIVYAWATA wilaya ya Meatu.
“ Tunaomba vifaa saidizi vya kukuza maandishi kwa wanafunzi wenye ualbino na pia walimu wawape nafasi ya kukaa mbele madarasani ili waweze kuona vizuri kama wanafunzi wengine kwa sababu wasipopata nafasi hiyo watashindwa kuona vizuri ubaoni kutokana na wao kuwa na uoni hafifu”Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye ualbino Meatu.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Festo Kiswaga amesema Serikali mkoani humo itaendelea kutoa kipaumbele kwa watu wenye uelemavu ambapo amesema wataendelea kujumuishwa katika agenda ya ujenzi wa uchumi wa viwanda kufikia uchumi wa kati mkoani humo.
Akiwa Wilayani Meatu, Mhe. Naibu Waziri amezungumza na viongozi, watu wenye ulemavu, kuona kazi mbalimbali za watu wenye ulemavu na kutembelea mradi wa Kitalu nyumba ili kujionea utekelezaji wake.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI :-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/02/serikali-kuzindua-mfuko-wa-watu-wenye.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa