Serikali imewahakikishia wakulima wa pamba Mkoani Simiyu kuwa itatoa chupa 2,000,000 za dawa ya kuuwa wadudu wanaoshambulia zao la Pamba ili kuwasaidia katika kukabiliana na wadudu hao.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe jana alipofanya ziara katika Wilaya ya Bariadi, Itilima na Maswa Mkoani Simiyu kwa ajili ya kukagua mashamba ya pamba na kujionea changamoto zinazowakabili wakulima wa pamba.
Mhandisi Mtigumwe amesema lengo la Serikali lilikuwa ni kutoa chupa za dawa 1,800,000 lakini kutokana kuongezeka kwa wakulima wa zao hilo, Serikali kupitia Bodi ya Pamba imeamua kutoa chupa 2,000,000 .
“Awali tulipanga kusambaza chupa 1,800,000 lakini mahitaji yamekuwa makubwa, kwa hiyo tutaongeza na kufikia chupa 2,000,000 na kufikia mwishoni mwa mwezi Februari chupa 1,000,000 zitakuwa zimeshafika Simiyu” alisistiza Mhandisi Mtigumwe.
Aidha, Mtigumwe alisisitiza viongozi na wataalam wa Kilimo mkoani Simiyu kusimamia ugawaji wa dawa hizo kwa wakulima na kuhakikisha zinatumika vizuri.
Aliongeza kuwa Wizara imetoa wataalam wake wasiopungua 60 kutoka makao makuu ya Wizara, Kituo cha Utafiti cha Ukirigulu na Chuo cha Kilimo Ukirigulu na kuwapeleka katika mikoa yote inayolima pamba, lengo likiwa ni kutoa elimu kwa wakulima na Maafisa Ugani juu ya matumizi sahihi ya dawa za kuua wadudu(viuadudu).
Masanja Mabula mkulima wa Pamba kutoka Kijiji cha Mbiti Wilayani Bariadi alisema katika msimu wa mwaka 2017/2018 wakulima wamehamasika kulima pamba hivyo wanaomba Serikali iwasaidie wapate dawa ili wadhibiti wadudu waharibifu.
Awali akiwasilisha taarifa ya Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini alisema Mkoa huo unahitaji chupa za dawa 1,810,839 kwa ajili ya wakulima wa pamba 309,511 ambao wamelima ekari 602,409 zikitarajiwa kuzalisha tani 421,686.3 za pamba kwa wastani wa kilo 700 kwa ekari moja.
Hadi kufikia Januari 31, 2018 Mkoa wa Simiyu umelima jumla ya hekta 241,445.2 sawa na ekari 603,613, ambazo ni asilimia 85.1 ya lengo la kulima ekari 709,296.5.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI JUU YA HABARI HII FUNGUA HAPA:-https://simiyuregion.blogspot.com/2018/02/serikali-kutoa-chupa-2000000-za-dawa-ya.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa