Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewaagiza Maafisa Utamaduni na Maafisa Maliasili wa Halmashauri zote mkoani humo kutambua vikundi vya Utamaduni vuinavyocheza ngoma zao na wanyama hai kama nyoka aina ya chatu na fisi ili viweze kuwekewa utaratibu wa kupata vibali vya Serikali.
Mtaka ameyasema hayo Julai 08, 2018 wakati akizungumza na wananchi katika Tamasha la SIMIYU JAMBO FESTIVAL Mjini Bariadi, ambalo limehusisha mashindano ya ngoma za asili (Wagika na Wagalu), mbio za baiskeli(Kilomita 150 wanaume na kilomita 100 wanawake), mbio fupi(Kilomita 10 na Kilometa tano), uandishi wa insha, likiwa limeshirikisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, nchi jirani ya Kenya.
Mtaka amesema yuko tayari kuwasaidia wanautamaduni hao ambao wanacheza ngoma zao na wanyama walio hai kulipia gharama zote za kupata vibali hivyo, ili waendelee kuutambuisha na tangaza utamaduni wa mkoa huo duniani.
“Nawaagiza maafisa Utamaduni na Maliasili wote kwenye halmashauri za Mkoa wa Simiyu wavitambue vikundi vyote vya utamaduni vinavyocheza na chatu, fisi na mtoe utaratibu wa kupata vibali vya kuwatumia wanyama hao, kama ni malipo mimi kama Mkuu wa Mkoa niko tayari kuwasaidia hao watu kulipa ili wawe kwenye utaratibu wa serikali” alisema Mtaka.
Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt Tulia Ackson ambaye alikuwa mageni Rasmi katika Simiyu Jambo Festival amesema suala la wanautamaduni kucheza na wanyama hai lipo maeneo mengi hapa nchini , hivyo akasisitiza kuwa ni vema suala la utaratibu wa kutoa vibali ukapatiwa ufumbuzi waweze kupewa vibali kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa ili kuwapa uhuru kufanya kazi zao.
“Hili jambo linapaswa kufanyiwa kazi, kama nilivyowaambia awali kuwa wenzetu wa Bujora Mwanza walipata fursa ya kwenda India kuonesha kazi zao za utamaduni na ngoma ya asili ambayo huwa wanacheza na nyoka lakini hawakufanikiwa kusafiri na nyoka kwa sababu ya changamoto ya kibali” alisema.
Tamasha la Simiyu Jambo Festival mwaka 2018 lilishirikisha washiriki kutoka mikoa 13 hapa nchini na nchi jirani ya Kenya huku likihusisha mashindano ya mbio za baiskeli (kilomita 150 wanaume, kilomita 100 wanawake, kilomita 10 walemavu), mashindano ya mbio fupi(kilomita 10 na kilomita tano), mashindano ya ngoma za asili(Wagika na Wagalu) na mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Bw. Mayunga Kidoyayi akionesha umahiri wake wa kucheza na manyama fisi wakati wa Tamasha la SIMIYU JAMBO FESTIVAL Mjini Bariadi, ambalo limehusisha mashindano ya ngoma za asili (Wagika na Wagalu), mbio za baiskeli(Kilomita 150 wanaume na kilomita 100 wanawake), mbio fupi(Kilomita 10 na Kilometa tano), uandishi wa insha, likiwa limeshirikisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, nchi jirani ya Kenya.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa