Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema Viongozi Mkoani Simiyu wataendelea kufanya kazi na kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia utawala bora, utawala unaofuata sheria na uongozi wa kuheshimiana na kusikilizana.
Mtaka ameyasema hayo Mei Mosi, 2019 wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi na wananchi mkoani humo katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Kimkoa, yaliyofanyika katika Uwanja wa Nguzonane Wilayani Maswa.
“Tungependa tujenge utumishi ambao ni wa kipekee sana kwenye mkoa na kila mtumishi aliye kwenye mkoa huu ajisikie fahari kufanya kazi Simiyu; ahadi yangu kwenu ni kwamba tutaendelea kufanya kazi kwa kuheshimiana,kusikilizana na kutiana moyo katikati ya changamoto ambazo watumishi wanazipitia” alisema
Aidha, amewashukuru wafanyakazi kwa namna walivyojitoa kwa hali na mali kuhakikisha kwamba malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi yanatekelezeka na kusisitiza kuwa mkoa utaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na Vyama vyote vya wafanyakazi na kuwataka waajiri wote wathamini vipaji vya watumishi wao.
Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Mkoa wa Simiyu, Bw. Said Mselem ameomba Serikali kushughulikia suala la upandaji wa mishahara na madaraja kwa watumishi ili kuwaongezea ari na motisha katika kazi.
Katika hatua nyingine Mselem ameiomba Serikali kuu kuona uwezekano wa kuwabadilishia mfumo wa malipo ya mshahara watumishi wanaolipwa kupitia mapato ya ndani na kuanza kuwalipa kupitia HAZINA, ili wawe na uhakika wa kupata mishahara yao na michango yao ya mifuko ya hifadhi ya jamii iwasilishwe kwa wakati.
Nao baadhi ya wafanyakazi kutoka vyama tofauti vya wafanyakazi wamesema Wafanyakazi Mkoani Simiyu wanapenda kazi zao na wanafanya kazi kwa uadilifu, hivyo wameiomba Serikali iendelee kuboresha mazingira na kuwasaidia kutatua changamtozao ili waweze kufanya kazi wa uhuru na kujituma zaidi.
‘Watumishi tunapenda kazi zetu na tunafanya kwa bidii na uadilifu, tunajua wapo wachache wanaotuangusha lakini tunaendelea kuwahimiza wawajibike kutimiza azma ya kuwatumikia wananchi, ombi letu kwa Serikali itukumbuke kwenye kupanda madaraja wapo ambao hawajapanda toka mwaka 2015” alisema Mwenyekiti CWT Itilima Mwl. Rehema Shalali.
“Watumishi wanaolipwa kwa mapato ya ndani wanakutana na changamoto ya mafao yao wanapostaafu, mafao hayaendi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwa wakati maana hawalipwi mishahara kwa wakati tunamwomba Mhe. Rais aliangalie hili, ili watumishi hao nao waweze kulipwa na HAZINA moja kwa moja” alisema Sara Kiyuga Mjumbe wa Baraza Kuu TALGWU Taifa.
Maadhimisho ya Mei Mosi kwa mwaka 2019 yamebebwa na Kauli Mbiu “ TANZANIA YA UCHUMI WA KATI INAWEZEKANA, WAKATI WA MISHAHARA NA MASLAHI BORA KWA WAFANYAKAZI NI SASA” ambapo yamefanyika kwa mara ya saba sasa Kimkoa tangu mkoa wa Simiyu kuanziswa mwezi Machi, 2012.
MWISHO
KUPATA PICHA ZAIDI KUHUSU HABARI HII TAFADHALI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/05/rc-mtaka-simiyu-tutaendelea-kufanya.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa