Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amewashauri wachezaji wa timu ya Coastal Union ya Tanga kutambua kuwa michezo ni biashara na pia ni ajira hivyo wanapaswa kujiwekea malengo ya muda mrefu na mfupi ili waweze kunufaika na matunda ya jitihada zao.
RC Mtaka ametoa kauli hiyo ofisini kwake mjini Bariadi alipotembelewa na kikosi cha timu hiyo na viongozi wake kilichokuwa kikitokea mkoani Mara kwenye mechi ya ligi kuu Tanzania Bara ambako ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa magoli 3 -2 na biashara United.
Katika salamu zake kwa timu hiyo Mtaka amesema njia pekee ya mafanikio kwa timu hiyo na wachezaji wake inaanzia kwenye nidhamu ya wachezaji ndani na nje ya uwanja na pia uwepo wa viongozi makini wanaojitambua na wenye nia ya kuleta mapinduzi ya soka nchini.
“ Binafsi sikubaliani na zile kauli mbiu za michezo ni afya au michezo ni burudani, naendelea kusisitiza michezo ni biashara halikadhalika michezo ni ajira hivyo kipaji chako ndio mtaji wako”.
“Mkitambua hilo mtafika mbali, tunayo mifano hai, hebu mtazameni mchezaji kama Mbwana Samatta, huyu alijitambua mapema, akajiwekea malengo na ndio maana ameweza kufikia hapo alipo,analipwa mshahara ambao watanzania wachache sana wanaupata”, aliongeza Mtaka.
“Kumbukeni nidhamu ndio muhimili mkubwa utakaowapeleka mbali,achaneni na ulimbukeni wa Usimba na Uyanga, na pia msikubali kuingia katika vishawishi vya kutumia dawa za kulevya, mkifanya hivyo kwa umri wenu huu nawahikikishia mtafika mbali kuliko mnavyotegemea”, alisisitiza RC Mtaka.
Aidha Mtaka pia aliwatolea mfano wachezaji wa zamani kama George Weah ambaye kwa sasa ni rais wa Liberia na golikipa wa zamani wa TP Mazembe Robert Kidiaba Muteba ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa mbunge huko Congo DRC kuwa ni kielelezo cha nidhamu bora michezoni akisema kuwa kama wangekuwa na sifa mbaya jamii isingeweza kukubali kuwapa nyadhifa kubwa za kisiasa.
Kuhusu uongozi wa vyama vya soka nchini, Mheshimiwa Mtaka amesema ipo haja ya kuvitazama kwa makini zaidi kwani kwa sehemu kubwa ya viongozi wake wanaendesha mambo kijanja kijanja hali inayodhoofisha jitihada za serikali za kuleta mapinduzi ya soka nchini.
“ Mara nyingi huwa najiuliza, hivi kuna haja gani ya kusajili mchezaji wa kigeni kwa mamilioni wakati kiwango chake ni cha chini kuliko wachezaji wetu wa ndani, hawa viongozi wana ajenda gani na soka letu mpaka kufikia maamuzi hayo”, alihoji Mtaka.
RC Mtaka ameongeza kuwa njia pekee itakayosaidia kuleta mabadiliko ya soka nchini ni mabadiliko ya mitazamo ya viongozi wake ambapo amesema wanapaswa kuweka uzalendo mbele na kuiona michezo kama fursa inayoweza kutangaza utalii wetu kupitia wachezaji waliowahi kutamba au wale wanaogonga vichwa vya habari hivi sasa akitolea mfano wa nchi kama Uganda ambayo baadhi ya mitaa yake imepewa majina ya wachezaji maarufu.
Aidha mheshimiwa Mtaka ambaye pia ni rais wa chama cha riadha nchini amesema kumekuwa na tofauti kubwa ya kimaisha kati ya wanariadha waliopata mafanikio kimichezo miaka ya nyuma na wachezaji wa soka waliowahi kutamba miaka hiyo kutokana na mfumo wa uongozi wa michezo uliopo.
RC Mtaka amesema kutokana na hali hiyo wachezaji wengi wa soka wamejikuta wakiwa taabani kimaisha mara baada ya kustaafu kucheza soka hali ambayo amesema tiba yake itapatikana endapo viongozi na wadau wa soka wataamua kubadili mitazamo yao na kuingia katika medani za soka la kibiashara kama ilivyo kwa nchi nyingi zilizoendelea.
Kwa upande wake kocha mkuu wa Coastal Union Juma Mgunda amekiri kuwepo kwa dosari za kiuongozi katika usimamizi wa mipango ya soka nchini na kuahidi kuufanyia kazi ushauri wake pale ambapo umeigusa timu yake.
“ Mheshimiwa mkuu wa mkoa timu yetu ni timu kongwe na imepitia vipindi vingi vya mpito, lakini kama ulivyojionea kwa sasa hali ni tofauti, tuna vijana chipukizi wenye uwezo mkubwa wa kuleta matokeo yatakayo washangaza wengi, binafsi ninaamini tutafika mbali”, aliongeza Mgunda.
Aidha kuhusu ushiriki wa mchezaji wa timu hiyo ambaye pia ni mwanamuziki maarufu wa kizazi kipya Ali Kiba, Mgunda amesema mchezaji huyo ni hazina kubwa ya timu hiyo na kwamba hawawezi kumtumia kwenye mechi za ugenini ambazo mapato yanachukuliwa na timu mwenyeji.
“Ali Kiba ni brand ya Coastal Union, anapoingia uwanjani ni lazima watu wajae kutazama mechi, na sisi kwa kutambua umuhimu wake tutamtumia kwa mechi za nyumbani tu ili pato lote liingie mfukoni kwetu”. Alisisitiza Mgunda.
Timu ya Coastal Union tayari imeondoka mjini Bariadi kuelekea Dar es Salaam kuendelea na michezo yake ya ligi kuu.
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa