Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Anthony Mtaka amesema mkoa huo utaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara ili waweze kunufaika na uwekezaji wanaoufanya ikiwa ni pamoja na kuchangia katika ukuaji pato la taifa.
Mhe. Mtaka ametoa kauli hiyo katika hafla ya uzinduzi wa hoteli ya kisasa ya Sweet Dreams mjini Bariadi na kusisitiza kuwa wafanyabiashara wanapaswa kuzibaini na kuzitumia kikamilifu fursa za kibiashara zilizopo ili waweze kujikwamua kiuchumi na pia kuharakisha maendeleo ya mkoa.
“Mwaka 2019 mkoa wetu utakuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kitaifa, kutakuwa na Nane Nane, Maonesho ya viwanda vidogo SIDO, Jukwaa la Ushirika na Siku ya mifuko ya hifadhi ya jamii, kumbukeni matukio yote haya yatakuja na wageni wengi watakaohitaji chakula, malazi na usafiri, mmejiandaaje kuitumia fursa hii,” alihoji Mhe Mtaka.
Halikadhalika Mhe Mtaka amewasisitiza wafanyabiashara mkoani humo kuhakikisha wanatoa huduma zenye ubora ili kuvutia wateja wengi zaidi kutoka ndani na nje ya mkoa jambo ambalo amesema litaongeza hamasa ya kuutangaza mkoa wa Simiyu.
Aidha kuhusu ukuaji wa sekta ya viwanda, mhe Mtaka ameongeza kuwa mapema mwaka 2019 mkoa unatarajiwa kuanza ujenzi wa viwanda vikubwa vitatu ikiwa ni pamoja na kiwanda cha vifaa tiba kitakachojengwa katika wilaya ya Bariadi pamoja na upanuzi wa kiwanda cha chaki na ujenzi wa kiwanda cha vifungashio mradi utakaotekelezwa wilayani Maswa huku akiwataka wafanyabiashara kuweka mikakati ya kunufaika na fursa hiyo.
“ Ujio wa miradi yote hii unategemea utayari wenu ninyi wafanyabiashara, endapo mnataka kunufaika na fursa zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hii fanyeni maandalizi mapema, mfano viwanda vyote nilivyovitaja vitaajiri watu zaidi ya elfu mbili na wote hawa watahitaji nyumba za kupanga, zitatakiwa hoteli na nyumba za wageni”, alisisitiza RC Mtaka.
Akijibu changamoto zilizobainishwa kwenye risala ya uongozi wa hoteli ya Sweet Dreams ikiwemo tatizo la maji pamoja na tatizo la kukatika umeme mara kwa mara, Mtaka ameuhakikishia uongozi wa hoteli hiyo kuwa serikali inazishughulikia ikiwa ni pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Lamadi unakamilika kwa wakati na pia amewahakikishia kuwa maandalizi ya kujenga kituo cha kupozea Umeme kitakacho maliza tatizo hilo yamekamilika.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mkoa wa Simiyu ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Itilima Mhe.Njalu Silanga amesema umoja huo utaendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano zinazoweka mazingira rafiki ya kufanya biashara akitolea mfano uamuzi wa serikali ya mkoa kuruhusu biashara kwa saa 24.
Kuhusu ushiriki wa wafanyabiashara kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi, Njalu ameongeza kuwa kutokana na elimu inayotolewa mara kwa mara anamini wafanyabiashara wamehamasika na wako tayari kushiriki kukuza uchumi wa taifa kwa kuzingatia sheria.
MWISHO
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa