Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wazazi, walimu na watumishi wengine wa Serikali, wanafunzi wa kike wanaopata mimba na jamii yote kwa ujumla kushirikiana na Serikali kuhakikisha wale wote waliowapa mimba wanafunzi wanabainika na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mtaka ameyasema hayo wakati akifunga kikao kazi cha viongozi na watendaji wa idara ya elimu kilichofanyika Machi 12, 2019 Mjini Bariadi kwa lengo la kuweka mikakati ya kuimarisha taaluma mkoa wa Simiyu.
Amesema katika uchunguzi wa awali uliofanyika imebainika kuwa wazazi, walimu, Maafisa Watendaji wa Kata na watumishi wengine wa Serikali na wanafunzi wenyewe waliopewa mimba wamekuwa wakikwamisha juhudi za serikali katika vita hii kwa kuwa sehemu ya kuharibu ushahidi.
“Kuna mimba zaidi ya 300 zimripotiwa katika maeneo mbalimbali baadhi ya maeneo wazazi wanashiriki kuharibu na wakati mwingine wanafunzi waliopata mimba wanashirikina na wazazi kuharibu ushahidi wa kesi wasi za wanafunzi wajawazito, baadhi ya maeneo walimu wetu wamehisiwa, kwingine watendaji wetu, naomba tushirikiane kuwabaini watu wanaowapa wanafunzi mimba kwenda kwenye hatua” alisema Mtaka..
Ameongeza kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa imekaa na wameshakubaliana hatua za kuchukua kwa wanafunzi, watumishi, wazazi na watu wote waliokatisha ndoto za wanafunzi wa kike kwa kuwapa mimba.
Kwa upande wake Mwalimu Huruma Mjinja kutoka Shule ya Sekondari Kidinda, amesema katika kukabiliana na tatizo la mimba kwa wanafunzi ni vema walimu na wazazi wakashirikiana kuwalinda watoto wa kike na wapate muda wa kuzungumza nao.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe, Anthony Mtaka amesema Wanafuzi wa kidato cha sita mkoani hapa wanatarajia kuanza kambi za kitaaluma rasmi Machi 31, 2019 kwa ajili ya kujiandaa na mtihani wa Taifa.
Aidha, Mtaka amewataka Wakuu wa shule za sekondari zenye wanafunzi wa kidato cha nne chini ya 25 kukutana na wazazi ili wakae na kukubaliana baadaye kuwakusanya wanafunzi hao kwa pamoja katika Shule ya sekondari Simiyu kwa ajili ya kufanya kambi za kitaaluma.
“Tunamaliza kujenga Simiyu Sekondari tukiwa na ziada ya vyumba vya madarasa 20 hivyo wakikaa watu 40 kwa kila chumba ni wanafunzi 800 tunajenga mabweni manne; shule zote za sekondari zenye wanafunzi wa kidato cha nne chini ya 25, bodi zao na viongozi wa Serikali wakae pamoja shuleni hapo kwa ajili ya kambi za kitaaluma baada ya likizo ya MweziAprili, 2019” alisema Mtaka.
Nao Baadhi ya Wakuu waShule wameahidi kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanafanya vizuri ili mkoa uweze kufanya vizuri pia kitaaluma huku akiomba viongozi wa mkoa waendelee kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vvizuri ili waweze kufanya vizuri zaidi kila mwaka.
“ Tutafanya jitihada kuhakikisha tunafanya vizuri lakini tunaomba viongozi wetu waendelee kuona haja ya kutoa motisha kwa wanaofanya vizuri kwa sababu mkiendelea kufanya hivyo mtatupa nguvu ya kufanya vizuri zaidi” Mwalimu Enelico Mwandibila kutoka wilaya ya Itilima.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju amesema mkoa huo umejiweka mkakati kabambe wa kuimarisha ufuatiliaji na ufundishaji na tathmini itafanyika kila mwezi kujua vipindi vilivyofundishwa na ambavyo havijafundishwa vitafidiwa.
Kikao hiki kimehudhuriwa na Maafisa Elimu na Taaluma wa Mkoa na Wilaya, baadhi ya Waratibu Elimu Kata, Wakuu wa Shule za Sekondari za Kidato cha Nne, wadhibiti ubora na baadhi ya wadau wa elimu mkoani Simiyu.
MWISHO.
KUPATA PICHA ZAIDI FUNGUA KIUNGANISHI HIKI:-https://simiyuregion.blogspot.com/2019/03/rc-mtaka-atoa-wito-kwa-jamii-kushiriki.html
Bariadi - Somanda
Anuani ya Posta: S. L. P. 4, BARIADI.
Simu ya Mezani: 028-2700011/2700054
Simu ya Mkononi: 028-2700011/2700054
Barua Pepe: ras@simiyu.go.tz
Hati Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu.Haki Zote Zimehifadhiwa